Sura

  1. 1
  2. 2
  3. 3
  4. 4
  5. 5
  6. 6
  7. 7
  8. 8
  9. 9
  10. 10
  11. 11
  12. 12
  13. 13
  14. 14
  15. 15
  16. 16
  17. 17
  18. 18
  19. 19
  20. 20
  21. 21
  22. 22
  23. 23
  24. 24
  25. 25
  26. 26
  27. 27
  28. 28
  29. 29
  30. 30
  31. 31
  32. 32
  33. 33
  34. 34
  35. 35
  36. 36
  37. 37
  38. 38
  39. 39
  40. 40
  41. 41
  42. 42
  43. 43
  44. 44
  45. 45
  46. 46
  47. 47
  48. 48
  49. 49
  50. 50
  51. 51
  52. 52

Agano la Kale

Agano Jipya

Yeremia 39 Biblia Habari Njema (BHN)

Kutekwa kwa mji wa Yerusalemu

1. Mnamo mwezi wa tisa wa mwaka wa tisa wa utawala wa Sedekia mfalme wa Yuda, Nebukadneza mfalme wa Babuloni alifika na jeshi lake lote kuushambulia mji wa Yerusalemu, akauzingira.

2. Na katika siku ya tisa ya mwezi wa nne, mwaka wa kumi na moja wa utawala wa Sedekia, sehemu ya ukuta wa mji ilibomolewa.

3. (Basi maofisa wakuu wafuatao wa mfalme wa Babuloni waliingia na kukaa kwenye lango la katikati: Nergal-shareza, Samgar-nebo, Sar-sekimu mkuu wa matowashi na Nergal-shareza mkuu wa wanajimu, pamoja na maofisa wengine wote wa mfalme wa Babuloni.)

4. Naye Sedekia, mfalme wa Yuda na askari wake wote walipowaona, walitoroka. Walitoka nje ya mji usiku, wakipitia katika bustani ya mfalme, kwenye lango katikati ya kuta mbili, wakaenda upande wa Araba.

5. Lakini jeshi la Wakaldayo liliwafuatia na kumteka Sedekia katika tambarare za Yeriko. Baada ya kumchukua walimfikisha kwa Nebukadneza, mfalme wa Babuloni huko Ribla, katika nchi ya Hamathi, naye akamhukumu.

6. Hukohuko Ribla, mfalme wa Babuloni aliwaua wana wa Sedekia mbele ya baba yao. Aliwaua pia maofisa wote wa Yuda.

7. Kisha alingoa macho yake Sedekia na kumfunga pingu, ili ampeleke Babuloni.

8. Wakaldayo waliichoma moto ikulu na nyumba za watu; pia walizibomoa kuta za Yerusalemu.

9. Kisha, Nebuzaradani, kapteni wa walinzi wa mfalme, aliwapeleka uhamishoni Babuloni watu waliokuwa wamebaki mjini na wale waliokuwa wamejisalimisha kwake pamoja na watu wote waliokuwa wamebaki.

10. Nebuzaradani, kapteni wa walinzi wa mfalme, aliwaacha katika nchi ya Yuda baadhi ya watu maskini ambao hawakuwa na chochote, akawagawia mashamba ya mizabibu na kuwapa maeneo ya kulima wakati huohuo.

Yeremia anafunguliwa

11. Nebukadneza mfalme wa Babuloni alikuwa amempa Nebuzaradani kapteni wa walinzi, amri ifuatayo kuhusu Yeremia:

12. “Mchukue Yeremia, umtunze vema wala usimdhuru; mtendee kama anavyokuambia.”

13. Basi, Nebuzaradani kapteni wa walinzi, Nebushani, Nergal-shareza pamoja na maofisa wakuu wote wa mfalme wa Babuloni, wakatuma watu wamtoe Yeremia ukumbini mwa walinzi.

14. Wakamkabidhi Yeremia kwa Gedalia mwana wa Ahikamu, mjukuu wa Shafani, amchukue nyumbani kwake. Basi, Yeremia akaishi pamoja na wananchi wengine.

Tumaini la Ebedmeleki

15. Neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Yeremia wakati alipokuwa amefungwa katika ukumbi wa walinzi:

16. “Nenda ukamwambie hivi Ebedmeleki, Mwethiopia: Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi: Tazama mimi nitatimiza mambo yale niliyotamka dhidi ya mji huo na sio mambo mema. Mambo hayo yatakamilika siku hiyo ukiona wewe mwenyewe.

17. Lakini siku hiyo mimi nitakuokoa wewe, wala hutatiwa mikononi mwa watu unaowaogopa.

18. Maana, kweli nitakuokoa na hutauawa vitani; utapata faida ya kuokoa maisha yako kwa sababu umeniamini mimi. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”