Sura

  1. 1
  2. 2
  3. 3
  4. 4
  5. 5
  6. 6
  7. 7
  8. 8
  9. 9
  10. 10
  11. 11
  12. 12
  13. 13
  14. 14
  15. 15
  16. 16
  17. 17
  18. 18
  19. 19
  20. 20
  21. 21
  22. 22
  23. 23
  24. 24
  25. 25
  26. 26
  27. 27
  28. 28
  29. 29
  30. 30
  31. 31
  32. 32
  33. 33
  34. 34
  35. 35
  36. 36
  37. 37
  38. 38
  39. 39
  40. 40
  41. 41
  42. 42
  43. 43
  44. 44
  45. 45
  46. 46
  47. 47
  48. 48
  49. 49
  50. 50
  51. 51
  52. 52

Agano la Kale

Agano Jipya

Yeremia 28 Biblia Habari Njema (BHN)

Yeremia na nabii Hanania

1. Mwaka uleule, mnamo mwezi wa tano wa mwaka wa nne wa utawala wa Sedekia mfalme wa Yuda, Hanania mwana wa Azuri, nabii kutoka mji wa Gibeoni, alisema nami katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Alisema nami mbele ya makuhani na watu wote, akaniambia,

2. “Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi: Nimeivunja nira ya mfalme wa Babuloni.

3. Mnamo miaka miwili nitavirudisha hapa vyombo vyote vya nyumba ya Mwenyezi-Mungu ambavyo Nebukadneza, mfalme wa Babuloni alivichukua na kuvipeleka Babuloni.

4. Pia nitamrudisha Yekonia mwana wa Yehoyakimu mfalme wa Yuda, pamoja na watu wote wa Yuda waliohamishiwa Babuloni. Naam, nitaivunja nira ya mfalme wa Babuloni. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”

5. Kisha, nabii Yeremia akamwambia nabii Hanania mbele ya makuhani na watu wote waliokuwa wamesimama katika hekalu la Mwenyezi-Mungu:

6. “Na iwe hivyo! Mwenyezi-Mungu na afanye hivyo. Mwenyezi-Mungu na ayatimize maneno uliyotabiri, avirudishe hapa vyombo vya nyumba ya Mwenyezi-Mungu kutoka Babuloni pamoja na watu wote waliohamishiwa huko.

7. Lakini sikiliza neno ninalokuambia wewe na watu wote.

8. Manabii waliotutangulia mimi na wewe, tangu zamani za kale, walitabiri kwamba vita, njaa na maradhi vitazikumba nchi nyingi na tawala kubwa.

9. Lakini nabii atabiriye amani, hutambuliwa tu kama nabii aliyetumwa na Mwenyezi-Mungu, ikiwa mambo aliyotabiri hutokea kweli.”

10. Ndipo nabii Hanania akaichukua ile nira shingoni mwa nabii Yeremia, akaivunja.

11. Naye Hanania akasema hivi mbele ya watu wote, “Mwenyezi-Mungu asema: Hivi ndivyo nitakavyovunja nira ambayo mfalme Nebukadneza ameyavisha mataifa yote; nitafanya hivyo mnamo miaka miwili ijayo.” Kisha nabii Yeremia akaenda zake.

12. Baada ya nabii Hanania kuvunja nira kutoka shingoni mwa nabii Yeremia, neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Yeremia:

13. “Nenda ukamwambie Hanania kwamba mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Wewe umevunja nira ya mti, lakini mimi nitatengeneza nyingine ya chuma.

14. Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, nasema kuwa nimeweka nira ya chuma ya utumwa shingoni mwa mataifa haya yote, nayo yatamtumikia Nebukadneza, mfalme wa Babuloni. Nimempa Nebukadneza hata wanyama wa porini wamtumikie.”

15. Basi, nabii Yeremia akamwambia nabii Hanania, “Sikiliza, Hanania, Mwenyezi-Mungu hakukutuma, nawe unawafanya watu hawa waamini uongo.

16. Kwa hiyo Mwenyezi-Mungu asema kwamba atakuondoa duniani. Mwaka huuhuu utakufa, kwa sababu umewaambia watu wamwasi Mwenyezi-Mungu.”

17. Mwaka huohuo, mnamo mwezi wa saba, nabii Hanania akafa.