Agano la Kale

Agano Jipya

Yeremia 36:11-29 Biblia Habari Njema (BHN)

11. Mikaia mwana wa Gemaria, mwana wa Shafani, aliposikia maneno yote ya Mwenyezi-Mungu ambayo yalisomwa kutoka kile kitabu,

12. alikwenda ikulu kwa mfalme katika chumba cha katibu walimokuwa wameketi wakuu wote: Katibu Elishama, Delaya mwana wa Shemaya, Elnathani mwana wa Akbori, Gemaria mwana wa Shafani, Sedekia mwana wa Hanania, na wakuu wote.

13. Mikaia aliwaambia maneno yote aliyoyasikia wakati Baruku aliposoma kitabu mbele ya umati wa watu.

14. Kisha, wakuu walimtuma Yehudi mwana wa Nethania, mjukuu wa Shelemia, kitukuu cha Kushi, amwambie Baruku hivi: “Chukua ile hati ya maandishi uliyosoma mbele ya watu uje nayo hapa.” Basi, Baruku mwana wa Neria, akachukua hati mkononi mwake, akawaendea.

15. Nao wakamwambia: “Keti, uisome.” Baruku akawasomea.

16. Waliposikia maneno hayo yote, walitazamana kwa hofu. Wakamwambia Baruku, “Hatuna budi kumweleza mfalme maneno haya yote.”

17. Kisha wakamwuliza Baruku, “Hebu tuambie, umepataje kuandika maneno yote haya? Je, Yeremia alisema, nawe ukayaandika?”

18. Baruku akawajibu: “Yeye alisema, nami nikawa nayaandika kwa wino katika hati hii.”

19. Kisha wakuu hao wakamwambia Baruku, “Wewe nenda ukajifiche pamoja na Yeremia, na pasiwe na mtu yeyote atakayejua mahali mlipo.”

20. Baada ya wakuu kuweka hati ile ndefu katika chumba cha Elishama katibu wa mfalme, walimwendea mfalme ukumbini, wakamjulisha mambo yote.

21. Kisha, mfalme alimtuma Yehudi aende kuleta ile hati. Yehudi aliichukua kutoka chumbani mwa katibu Elishama, akamsomea mfalme na wakuu wote waliokuwa wamesimama karibu na mfalme.

22. Wakati huo ulikuwa mwezi wa tisa, na mfalme alikuwa ndani ya nyumba yake ya majira ya baridi, akiota moto wa makaa.

23. Ikawa, mara baada ya Yehudi kusoma safu tatu au nne hivi za hiyo hati ndefu, mfalme alizikata safu hizo kwa kisu na kuzitupa katika moto wa makaa. Aliendelea kufanya hivyo mpaka hati yote ikateketea.

24. Lakini, ingawa mfalme na watumishi wake wote waliyasikia maneno hayo yote, hawakuogopa wala kuyararua mavazi yao kwa huzuni.

25. Ijapokuwa Elnata, Delaya na Gemaria walimsihi mfalme asiichome hati hiyo, mfalme hakuwasikiliza.

26. Mfalme alimwamuru Yerameeli mwanawe, Seraya mwana wa Azrieli na Shelemia mwana wa Abdeli, wamkamate katibu Baruku na nabii Yeremia. Lakini Mwenyezi-Mungu aliwaficha.

27. Baada ya mfalme kuchoma moto hati ile ya maneno aliyoandika Baruku kwa maagizo ya Yeremia, neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Yeremia:

28. “Chukua hati nyingine ndefu, uandike maneno yote yaliyokuwa katika ile hati ya kwanza ambayo Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, ameichoma moto.

29. Na huyo Yehoyakimu mfalme wa Yuda, wewe utamwambia kuwa mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Yeye ameichoma moto hati hiyo na kuuliza kwa nini Yeremia ameandika kwamba mfalme wa Babuloni atakuja kuiharibu nchi hii na kuwaangamiza watu na wanyama!

Kusoma sura kamili Yeremia 36