Agano la Kale

Agano Jipya

Yeremia 29:3-22 Biblia Habari Njema (BHN)

3. Barua hii ilipelekwa na Elasa mwana wa Shafani, na Gemaria mwana wa Hilkia, ambao Sedekia, mfalme wa Yuda, aliwatuma kwa Nebukadneza mfalme wa Babuloni. Yeremia aliandika hivi:

4. “Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi kuhusu mateka wote aliowaacha wachukuliwe kutoka Yerusalemu hadi Babuloni:

5. ‘Jengeni nyumba mkae. Limeni mashamba, pandeni mbegu na kula mazao yake.

6. Oeni wake, mpate watoto; waozeni wana wenu na binti zenu nao pia wapate watoto. Ongezekeni na wala msipungue.

7. Shughulikieni ustawi wa mji ambamo nimewahamishia. Niombeni kwa ajili ya mji huo, maana katika ustawi wake nyinyi mtastawi.

8. Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, nasema hivi: Msikubali kudanganywa na manabii wenu na waaguzi waliomo miongoni mwenu, wala msisikilize ndoto wanazoota.

9. Maana wanawatabiria uongo kwa kutumia jina langu. Mimi sikuwatuma. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.’

10. “Mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Baada ya miaka sabini huko Babuloni, baada ya muda huo, nitawajia na kuitimiza ahadi yangu ya kuwarudisha mahali hapa.

11. Maana, mimi Mwenyezi-Mungu ninajua mambo niliyowapangia. Nimewapangieni mema na si mabaya, ili mpate kuwa na tumaini la baadaye.

12. Hapo ndipo mtakaponiita na kuniomba, nami nitawasikiliza.

13. Mtanitafuta na kunipata. Mtakaponitafuta kwa moyo wote

14. mtanipata. Nami nitawarudishieni fanaka zenu na kuwakusanya kutoka mataifa yote na mahali pote nilipowafukuzia. Nitawarudisheni mahali ambapo niliwatoa, nikawapeleka uhamishoni. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.

15. “Nyinyi mnawasadiki manabii ambao mwasema kwamba Mwenyezi-Mungu amewaleteeni huko Babuloni.

16. Sikilizeni nisemavyo mimi Mwenyezi-Mungu kuhusu mfalme anayekalia kiti cha enzi cha Daudi, na kuhusu watu wote wanaokaa katika mji huu, na ndugu zenu ambao hawakuondoka pamoja nanyi kwenda uhamishoni.

17. Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nasema hivi: Tazama, ninawapelekea upanga, njaa na maradhi mabaya; nitawafanya kuwa kama tini mbaya sana, hata haziwezi kuliwa.

18. Nitawaandama kwa upanga, njaa na maradhi mabaya. Nitawafanya kuwa kitu cha kuchukiza kwa tawala zote za dunia, naam, kitu cha laana, kioja, dharau na kitu cha kupuuzwa katika mataifa yote nilikowafukuzia.

19. Nitafanya hivyo kwa sababu hamkusikiliza maneno yangu niliyowaambia kila mara kwa njia ya watumishi wangu, manabii, nanyi mkakataa kusikiliza. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.

20. Enyi nyote niliowatoa kutoka Yerusalemu, nikawapeleka uhamishoni Babuloni, sikilizeni neno langu mimi Mwenyezi-Mungu.”

21. Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli asema hivi juu ya Ahabu mwana wa Kolaya, na juu ya Sedekia mwana wa Maaseya, ambao wanawatabirieni uongo kwa jina lake: “Nitawatia mikononi mwa Nebukadneza, mfalme wa Babuloni, naye atawaua mkiona kwa macho yenu wenyewe.

22. Kwa sababu jambo hilo litakalowapata, watu wote waliohamishiwa Babuloni kutoka Yerusalemu watatumia msemo huu wa kulaania: Mwenyezi-Mungu akufanye kama Sedekia na Ahabu, ambao mfalme wa Babuloni aliwachoma motoni.

Kusoma sura kamili Yeremia 29