Agano la Kale

Agano Jipya

2 Wafalme 14:10-23 Biblia Habari Njema (BHN)

10. Sasa wewe Amazia umewashinda kabisa Waedomu, na moyo wako unakufanya ujivune. Ridhika na utukufu wako, ukakae nyumbani; ya nini kujitafutia taabu zitakazokuangamiza wewe mwenyewe pamoja na watu wako wa Yuda?”

11. Lakini Amazia hakujali. Kwa hiyo Yehoashi mfalme wa Israeli alitoka akakabiliana uso kwa uso na Amazia huko vitani Beth-shemeshi, nchini Yuda.

12. Watu wa Yuda walishindwa na watu wa Israeli na kila mmoja alirudi kwake.

13. Yehoashi mfalme wa Israeli alimteka Amazia mfalme wa Yuda, mwana wa Yehoashi, mwana wa Ahazia huko Beth-shemeshi; halafu akauendea Yerusalemu na kuubomoa ukuta wake kutoka Lango la Efraimu mpaka Lango la Pembeni, umbali wa karibu mita 200.

14. Alichukua dhahabu yote na fedha, hata na vifaa vyote vilivyokuwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu na katika hazina ya ikulu; pia alichukua mateka, kisha akarudi Samaria.

15. Matendo mengine yote ya Yehoashi, ushujaa wake na vita alivyopigana na mfalme Amazia wa Yuda yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Israeli.

16. Yehoashi alifariki, akazikwa katika makaburi ya kifalme huko Samaria. Mwanae, Yeroboamu akatawala mahali pake.

17. Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda aliishi miaka kumi na mitano baada ya mfalme Yehoashi wa Israeli kufariki.

18. Matendo mengine yote ya Amazia yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Yuda.

19. Njama za kumwua Amazia zilifanywa Yerusalemu, kwa hiyo alikimbilia Lakishi, lakini maadui walituma watu wa kumwua huko.

20. Maiti yake ililetwa juu ya farasi na kuzikwa katika makaburi ya kifalme katika Yerusalemu katika mji wa Daudi.

21. Kisha watu wote wa Yuda wakamchukua Azaria akiwa na umri wa miaka kumi na sita, wakamtawaza mahali pa Amazia baba yake.

22. Azaria, baada ya kifo cha baba yake, aliujenga upya mji wa Elathi na kuurudisha kwa Yuda.

23. Katika mwaka wa kumi na tano wa enzi ya Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda, Yeroboamu mwana wa Yehoashi mfalme wa Israeli alianza kutawala huko Samaria, akatawala kwa muda wa miaka arubaini na mmoja.

Kusoma sura kamili 2 Wafalme 14