Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wafalme 22:17-31 Biblia Habari Njema (BHN)

17. Ndipo, Mikaya akasema, “Niliona watu wote wa Israeli wametawanyika milimani kama kondoo wasio na mchungaji. Naye Mwenyezi-Mungu akasema, ‘Watu hawa hawana kiongozi; basi warudi kila mtu nyumbani kwake kwa amani.’”

18. Hapo, mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, “Sikukuambia kamwe hatatabiri jema juu yangu ila mabaya tu?”

19. Kisha Mikaya akasema, “Haya sikia neno la Mwenyezi-Mungu: Nilimwona Mwenyezi-Mungu ameketi katika kiti chake cha enzi, na jeshi lote la mbinguni limesimama kando yake, upande wake wa kulia na wa kushoto;

20. ndipo Mwenyezi-Mungu akauliza, ‘Ni nani atakayemshawishi Ahabu aende akaangamie huko Ramoth-gileadi?’ Kila mmoja akajibu alivyofikiri.

21. Kisha pepo mmoja akajitokeza mbele ya Mwenyezi-Mungu, akasema, ‘Mimi nitamshawishi.’

22. Mwenyezi-Mungu akamwuliza, ‘Kwa mbinu gani?’ Naye akajibu, ‘Nitakwenda na kuwafanya manabii wake wote waseme uongo.’ Mwenyezi-Mungu akamwambia, ‘Wewe utamshawishi na utafaulu; haya, nenda ukafanye hivyo.’

23. Basi, ndivyo ilivyo: Mwenyezi-Mungu amewafanya hawa manabii wako wote waseme uongo. Mwenyezi-Mungu amenena mabaya juu yako!”

24. Hapo, Sedekia, mwana wa Kenaana, akamkaribia Mikaya, akampiga kofi shavuni na kumwuliza, “Tangu lini Roho ya Mwenyezi-Mungu ikaniacha mimi, ikaja kunena nawe?”

25. Mikaya akamjibu, “Siku utakapoingia katika chumba cha ndani kujificha, ndipo utakapojua.”

26. Naye mfalme wa Israeli akatoa amri, “Mkamateni Mikaya; mrudisheni kwa Amoni, mkuu wa mji, na kwa Yoashi mwana wa mfalme.

27. Waambie wamtie gerezani na kumlisha mkate kidogo na maji, mpaka nitakaporudi salama.”

28. Ndipo Mikaya aliposema, “Ukirudi salama basi, utajua kwamba Mwenyezi-Mungu hakunena nami.” Kisha akaendelea kusema, “Sikilizeni enyi watu wote!”

29. Basi, mfalme wa Israeli akaenda pamoja na mfalme Yehoshafati wa Yuda, kuushambulia mji wa Ramoth-gileadi.

30. Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, “Mimi nitavaa mavazi yasiyo ya kifalme na kuingia vitani lakini wewe utavaa mavazi yako ya kifalme.” Hivyo mfalme wa Israeli akaenda vitani bila kuvaa mavazi ya kifalme.

31. Mfalme wa Aramu alikuwa amewaamuru makapteni wake thelathini na wawili waliosimamia magari yake ya kukokotwa, akisema: “Msipigane na mtu yeyote yule, mkubwa au mdogo, ila tu na mfalme wa Israeli.”

Kusoma sura kamili 1 Wafalme 22