Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wafalme 20:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Ben-hadadi mfalme wa Aramu, alikusanya jeshi lake lote; aliungwa mkono na wafalme wengine thelathini na wawili pamoja na farasi na magari yao ya kukokotwa. Aliuendea mji wa Samaria akauzingira na kuushambulia.

2. Kisha, akatuma wajumbe wake mjini kwa mfalme Ahabu wa Israeli, wakamwambia, “Mfalme Ben-hadadi asema hivi:

3. ‘Fedha na dhahabu yako yote ni mali yangu; wake zako warembo na watoto wako pia ni wangu.’”

4. Naye mfalme wa Israeli akajibu, “Bwana wangu mfalme, ulivyosema ni sawa: Mimi ni wako, na vyote nilivyo navyo ni vyako.”

5. Baadaye, wajumbe hao wakamrudia tena Ahabu, wakamwambia, “Mfalme Ben-hadadi asema hivi: ‘Nilikutumia ujumbe unipe dhahabu, fedha, wake zako pamoja na watoto wako.

6. Sasa, kesho wakati kama huu, nitatuma watumishi wangu waje kuisaka ikulu na nyumba za watumishi wako, wachukue kila kitu unachothamini.’”

7. Ndipo Ahabu mfalme wa Israeli, akawaita viongozi wote wa nchi, akawaambia, “Sasa, oneni jinsi jamaa huyu anavyotaka kututaabisha! Ametuma ujumbe kwamba anataka wake zangu, watoto wangu, dhahabu na fedha yangu. Nami sikumkatalia!”

8. Wazee na watu wote wakamwambia, “Usimjali wala usikubali.”

9. Basi, Ahabu akawaambia wajumbe wa Ben-hadadi, “Mwambieni bwana wangu mfalme hivi: ‘Niko radhi kutimiza matakwa yako ya kwanza, lakini haya ya pili sikubali hata kidogo.’” Hapo, wajumbe hao wakaenda zao na kumhabarisha tena mfalme Ben-hadadi.

10. Ben-hadadi akamtumia Ahabu ujumbe huu: “Miungu na waniulie mbali, nakuapia, ikiwa huko Samaria kutabakia mavumbi ya kutosha gao moja kwa kila mmoja wa watu wangu wengi!”

11. Mfalme Ahabu wa Israeli akajibu, “Mwambieni mfalme Ben-hadadi kwamba shujaa hujisifu baada ya vita, si kabla!”

12. Ben-hadadi alipokea ujumbe huu wa Ahabu wakati yeye na wafalme waliomwunga mkono walipokuwa mahemani mwao wanakunywa. Basi, akayaweka majeshi yake katika hali ya tahadhari, kuushambulia mji.

13. Wakati huohuo, nabii mmoja akamwendea Ahabu, mfalme wa Israeli, akamwambia, “Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Unaona wingi wa majeshi haya? Leo hii nitawatia mikononi mwako, nawe utatambua kwamba mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.’”

Kusoma sura kamili 1 Wafalme 20