Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wafalme 12:11-20 Biblia Habari Njema (BHN)

11. Mzigo wa baba yangu ulikuwa mzito, lakini wangu utakuwa mzito zaidi. Baba yangu aliwapiga kwa mijeledi, lakini mimi nitawapiga kwa mijeledi yenye miiba.’”

12. Basi, siku ya tatu Yeroboamu pamoja na watu wote wakarudi kwa Rehoboamu kama alivyokuwa amewaagiza.

13. Mfalme akawajibu watu hao kwa ukali, akapuuza shauri alilopewa na wazee,

14. akafuata shauri la vijana wenzake, akawaambia, “Baba yangu aliwatwika mzigo mzito, lakini mimi nitaufanya kuwa mzito zaidi. Baba yangu aliwapiga kwa mijeledi, lakini mimi nitawapiga kwa mijeledi yenye miiba.”

15. Hivyo, mfalme hakuwajali watu kwa sababu jambo hili lilisababishwa na Mwenyezi-Mungu, ili atimize neno lake alilomwambia Yeroboamu mwana wa Nebati, kwa njia ya Ahiya wa Shilo.

16. Lakini watu wote wa Israeli walipoona kwamba mfalme hakuwajali, walimwambia,“Hatuna uhusiano wowote na Daudi!Hatuna sehemu yetu kutoka kwa huyo mwana wa Yese.Rudini nyumbani, enyi watu wa Israeli!Itunze nyumba yako mwenyewe, ee Daudi.”Hivyo, watu wa Israeli wakarudi makwao.

17. Watu wa Israeli waliokuwa wanakaa katika miji ya Yuda, ndio hao tu waliobaki chini ya utawala wa Rehoboamu.

18. Mfalme Rehoboamu alipomtuma Adoramu, aliyekuwa mnyapara mkuu wa kazi za kulazimishwa, watu wote wa Israeli walimpiga mawe, wakamuua. Naye Rehoboamu alipanda haraka gari lake la kukokotwa, akakimbilia Yerusalemu.

19. Hivyo watu wa Israeli wamekuwa katika hali ya uasi dhidi ya ukoo wa Daudi mpaka leo.

20. Watu wote wa Israeli walipopata habari kwamba Yeroboamu alikuwa amerudi kutoka Misri, walimwita katika mkutano wa hadhara, wakamtawaza kuwa mfalme wa Israeli yote. Hakuna kabila lingine lililojiunga na ukoo wa Daudi isipokuwa tu kabila la Yuda.

Kusoma sura kamili 1 Wafalme 12