Agano la Kale

Agano Jipya

2 Wafalme 18:6-21 Biblia Habari Njema (BHN)

6. Yeye hakumwasi Mwenyezi-Mungu wala hakuacha kumfuata, bali alishika amri za Mwenyezi-Mungu alizomwamuru Mose.

7. Basi, Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja naye, na alimfanya kufaulu kwa kila alilotenda. Alimwasi mfalme wa Ashuru na kukataa kumtumikia.

8. Aliwapiga Wafilisti mpaka mji wa Gaza na nchi iliyouzunguka, kuanzia mnara wa walinzi mpaka mji wenye ngome.

9. Katika mwaka wa nne wa enzi ya Hezekia, ambao pia ulikuwa mwaka wa saba wa enzi ya Hoshea mwana wa Ela mfalme wa Israeli, Shalmanesa mfalme wa Ashuru alishambulia mji wa Samaria na kuuzingira.

10. Mwishoni mwa mwaka wa tatu Waashuru waliuteka Samaria. Ilikuwa katika mwaka wa sita wa enzi ya Hezekia na pia mwaka wa tisa wa enzi ya Hoshea mfalme wa Israeli, Samaria ulipotekwa.

11. Mfalme wa Ashuru aliwachukua watu wa Israeli mateka mpaka Ashuru na kuwaweka wengine wao katika mji wa Hala, na karibu ya Habori, mji wa Gozani, pia na wengine katika miji ya Media,

12. kwa sababu Waisraeli hawakutii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, bali walivunja agano lake, hata hawakusikia wala kutii yote Mose, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, aliyowaamuru.

13. Mnamo mwaka wa kumi na nne wa utawala wa mfalme Hezekia, mfalme Senakeribu wa Ashuru aliishambulia miji yote yenye ngome ya Yuda na kuiteka.

14. Hezekia akatuma ujumbe kwa Senakeribu huko Lakishi na kumwambia, “Nimefanya makosa. Tafadhali, komesha mashambulio yako kwangu; nami nitalipa chochote utakacho.” Mfalme wa Ashuru akaagiza Hezekia amletee tani kumi za fedha na tani moja ya dhahabu.

15. Hezekia akampelekea fedha yote iliyokuwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu na katika hazina za nyumba ya mfalme;

16. kadhalika, alingoa dhahabu kutoka katika milango ya hekalu la Mwenyezi-Mungu na ile dhahabu ambayo yeye mwenyewe aliiweka kwenye mihimili ya mlango; yote akampelekea Senakeribu.

17. Kisha mfalme wa Ashuru alimtuma jemadari mkuu, amiri mkuu, mkuu wa matowashi pamoja na jeshi kubwa kutoka Lakishi kwenda kwa mfalme Hezekia huko Yerusalemu. Walisafiri na kufika Yerusalemu. Nao walipowasili waliingia na kusimama karibu na mfereji wa bwawa lililoko upande wa juu katika barabara kuu inayoelekea Uwanda wa Dobi.

18. Walipomwita mfalme Hezekia walilakiwa na Eliakimu mwana wa Hilkia, ambaye alikuwa msimamizi wa ikulu; Shebna, aliyekuwa katibu na Yoa mwana wa Asafu, mwandishi wa kumbukumbu za mfalme.

19. Ndipo jemadari mkuu alipowaambia, “Mwambieni Hezekia, hivi ndivyo anavyosema mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru: Ni ujasiri wa namna gani huu unaouwekea matumaini?

20. Je, unadhani kuwa maneno matupu ndiyo maarifa na nguvu katika vita? Ni nani unayemtegemea hata ukaniasi?

21. Angalia, sasa, unategemea Misri, utete uliovunjika ambao utamchoma mkono yeyote atakayeutegemea. Hivyo ndivyo Farao mfalme wa Misri alivyo kwa wote wale wanaomtegemea.”

Kusoma sura kamili 2 Wafalme 18