Agano la Kale

Agano Jipya

2 Wafalme 17:20-35 Biblia Habari Njema (BHN)

20. Mwenyezi-Mungu aliwakataa Waisraeli wote; akawaadhibu na kuwaacha mikononi mwa adui wakali, na kisha akawafukuza mbele yake.

21. Baada ya Mwenyezi-Mungu kutenga watu wa Israeli kutoka ukoo wa Daudi, walimtawaza Yeroboamu mwana wa Nebati kuwa mfalme. Naye Yeroboamu aliwafanya watu wa Israeli kumwacha Mwenyezi-Mungu na kutenda dhambi kubwa sana.

22. Waisraeli walitenda dhambi alizotenda Yeroboamu; hawakuweza kuziacha,

23. hadi hatimaye Mwenyezi-Mungu akawafukuza kutoka mbele yake, kama vile alivyokuwa amesema kupitia kwa watumishi wake wote manabii. Kwa hiyo watu wa Israeli walichukuliwa mateka kutoka nchi yao wenyewe mpaka Ashuru ambako wanakaa hata sasa.

24. Kisha mfalme wa Ashuru akachukua watu kutoka Babuloni, Kutha, Ava, Hamathi na Sefarvaimu na kuwaweka katika miji ya Samaria mahali pa watu wa Israeli waliopelekwa uhamishoni. Wakaitwaa miji hiyo na kukaa humo.

25. Basi ilitokea kwamba walipoanza kukaa humo, hawakumwabudu Mwenyezi-Mungu, kwa hiyo Mwenyezi-Mungu akatuma simba miongoni mwao, nao wakawaua baadhi yao.

26. Halafu watu walimwambia mfalme wa Ashuru, “Mataifa uliyochukua na kuyaweka katika miji ya Samaria hayakujua hukumu za Mungu wa nchi hiyo, kwa hiyo Mungu huyo alituma simba ambao wanawaua.”

27. Ndipo mfalme wa Ashuru akaamuru, “Mrudishe kuhani mmoja kati ya wale tuliowaleta mateka; mrudishe aende na kukaa huko, ili awafundishe watu sheria ya Mungu wa nchi hiyo.”

28. Kwa hiyo mmoja wa makuhani waliotekwa nyara toka Samaria alikwenda na kukaa Betheli, na huko aliwafundisha watu jinsi ya kumwabudu Mwenyezi-Mungu.

29. Lakini mataifa yote katika miji yalimoishi yalijitengenezea miungu yao na kuiweka mahali pa juu ambako watu wa Samaria walikuwa wametengeneza.

30. Watu wa Babuloni walitengeneza vinyago vya Sukoth-benothi; Wakuthi vinyago vya Nergali; Wahamathi vinyago vya Ashima;

31. Waiva vinyago vya Nibhazi na Tartaki; na Wasefarvaimu walitoa watoto wao kuwa sadaka za kuteketezwa kwa miungu yao Adrameleki na Anameleki.

32. Watu hawa vilevile walimwabudu Mwenyezi-Mungu. Waliteua kutoka kati yao watu wa kila aina na kuwafanya makuhani kutumika katika mahali pa juu na kutoa sadaka huko kwa niaba yao.

33. Hivi walimwabudu Mwenyezi-Mungu, lakini wakati huohuo waliwaabudu pia miungu yao waliyoichukua kutoka nchi zao.

34. Hata sasa wanatenda kama walivyofanya hapo awali. Hawamwabudu Mwenyezi-Mungu, na wala hawafuati masharti, maagizo, sheria au amri ambazo yeye Mwenyezi-Mungu aliwaamuru wana wa Yakobo; ambaye alimpa jina Israeli.

35. Mwenyezi-Mungu alikuwa amefanya agano nao na kuwaamuru, “Msiabudu miungu mingine; msiisujudie, msiitumikie wala msiitambikie.

Kusoma sura kamili 2 Wafalme 17