Agano la Kale

Agano Jipya

2 Wafalme 14:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Katika mwaka wa pili wa enzi ya Yehoashi mwana wa Yehoahazi huko Israeli, Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda alianza kutawala.

2. Alipoanza kutawala alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano, naye alitawala katika Yerusalemu kwa muda wa miaka ishirini na tisa. Mama yake aliitwa Yehoadani wa Yerusalemu.

3. Alitenda yaliyo mema mbele ya Mwenyezi-Mungu, lakini hakuwa kama babu yake Daudi. Bali alifanya mambo yote kama Yoashi baba yake;

4. isipokuwa mahali pa ibada milimani hapakuharibiwa na watu waliendelea kutambika na kufukiza ubani mahali hapo.

5. Mara tu Amazia alipojiimarisha mamlakani, aliwaua watumishi waliomuua mfalme, baba yake.

6. Lakini hakuwaua watoto wa wauaji; kama ilivyoandikwa katika Kitabu cha Sheria za Mose, Mwenyezi-Mungu anapotoa amri akisema, “Wazazi hawatauawa kwa ajili ya watoto wao, wala watoto hawatauawa kwa ajili ya wazazi wao; bali kila mtu atauawa kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe.”

7. Amazia aliwaua Waedomu 10,000 katika Bonde la Chumvi; aliutwaa kwa nguvu mji wa Sela na kuuita Yoktheeli, na hivi ndivyo unavyoitwa mpaka sasa.

8. Kisha Amazia akatuma wajumbe kwa Yehoashi mwana wa Yehoahazi, mwana wa Yehu mfalme wa Israeli akisema, “Njoo tupambane.”

9. Lakini Yehoashi mfalme wa Israeli alimpelekea ujumbe Amazia mfalme wa Israeli, akisema, “Siku moja mbaruti wa Lebanoni uliuambia mwerezi, wa huko Lebanoni pia, ‘Mwoze binti yako kwa mwanangu.’ Lakini mnyama wa mwituni akapita hapo na kuukanyagakanyaga mbaruti huo.

10. Sasa wewe Amazia umewashinda kabisa Waedomu, na moyo wako unakufanya ujivune. Ridhika na utukufu wako, ukakae nyumbani; ya nini kujitafutia taabu zitakazokuangamiza wewe mwenyewe pamoja na watu wako wa Yuda?”

11. Lakini Amazia hakujali. Kwa hiyo Yehoashi mfalme wa Israeli alitoka akakabiliana uso kwa uso na Amazia huko vitani Beth-shemeshi, nchini Yuda.

12. Watu wa Yuda walishindwa na watu wa Israeli na kila mmoja alirudi kwake.

Kusoma sura kamili 2 Wafalme 14