Agano la Kale

Agano Jipya

2 Wafalme 13:12-22 Biblia Habari Njema (BHN)

12. Matendo mengine yote ya Yehoashi, ushujaa wake na vita alivyopigana na mfalme Amazia wa Yuda, yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Israeli.

13. Yehoashi alifariki na kuzikwa katika makaburi ya kifalme huko Samaria, naye mwanawe Yeroboamu wa pili akatawala mahali pake.

14. Nabii Elisha aliugua ugonjwa mbaya sana. Alipokuwa karibu kufa, mfalme Yehoashi wa Israeli alimtembelea. Alipomfikia Elisha, alilia, akisema, “Baba yangu, baba yangu! Magari ya Israeli na wapandafarasi wake!”

15. Elisha akamwamuru, “Hebu lete upinde na mishale!” Yehoashi akavileta.

16. Elisha akamwambia ajitayarishe kupiga mishale. Mfalme akajitayarisha na Elisha akaiweka mikono yake juu ya mikono ya mfalme.

17. Mfalme alifuata maagizo ya nabii na kufungua dirisha ambalo lilielekea Aramu. Elisha akatoa amri “Tupa mshale!” Mara tu mfalme alipotupa mshale, nabii akasema, “Wewe ndio mshale wa Mwenyezi-Mungu, ambao kwao atapata ushindi juu ya Waaramu. Utapigana na Waaramu huko Afeka mpaka uwashinde.”

18. Ndipo Elisha akamwambia mfalme achukue mishale mingine na kuipiga chini. Mfalme akapiga mishale chini mara tatu, kisha akaacha.

19. Elisha alikasirika sana, akamwambia mfalme, “Mbona hukupiga mara tano au sita? Hivyo ungewaangamiza Waaramu kabisa. Lakini sasa utawashinda mara tatu tu.”

20. Elisha alifariki, akazikwa.Kila mwaka, makundi ya Wamoabu yalikuja kuishambulia nchi ya watu wa Israeli.

21. Wakati mmoja, wakati wa mazishi, watu waliona kundi mojawapo la watu waliobeba maiti wakamtupa yule maiti kaburini mwa Elisha na kukimbia. Mara maiti huyo alipogusa mifupa ya Elisha, alifufuka na kusimama wima.

22. Mfalme Hazaeli wa Aramu aliwanyanyasa sana watu wa Israeli wakati wote wa enzi ya Yehoahazi.

Kusoma sura kamili 2 Wafalme 13