Agano la Kale

Agano Jipya

2 Samueli 19:8-26 Biblia Habari Njema (BHN)

8. Kisha, mfalme akatoka akaenda, akaketi mahali pake karibu na lango. Watu wote walipoambiwa kuwa mfalme yuko langoni, wote walimwendea.Wakati huo, watu wote wa Israeli walikuwa wamekimbia, kila mmoja nyumbani kwake.

9. Watu wote walikuwa wanashindana wao kwa wao katika makabila yote ya Israeli, wakisema, “Mfalme Daudi alitukomboa mikononi mwa adui zetu, alituokoa mikononi mwa Wafilisti. Lakini sasa ameikimbia nchi, akimkimbia Absalomu.

10. Tena Absalomu ambaye tulimpaka mafuta awe mfalme wetu, sasa ameuawa vitani. Sasa, kwa nini hatuzungumzii juu ya kumrudisha mfalme Daudi?”

11. Mfalme Daudi akatuma ujumbe kwa makuhani Sadoki na Abiathari, “Waambieni wazee wa Yuda: ‘Kwa nini wao wawe ndio wa mwisho kumrudisha mfalme nyumbani kwake? Ujumbe wa Israeli yote umenifikia mimi mfalme.

12. Nyinyi ni ndugu zangu, nyinyi ni damu yangu; kwa nini muwe wa mwisho kunirudisha mimi mfalme nyumbani?

13. Mwulizeni pia Amasa kama yeye si damu yangu. Tena Mungu aniue ikiwa simfanyi yeye kuwa kamanda wa jeshi langu tangu leo badala ya Yoabu.’”

14. Hivyo, Daudi aliivuta mioyo ya watu wote wa Yuda kama mtu mmoja. Hivyo, wakampelekea ujumbe kusema “Rudi nyumbani, wewe na watumishi wako wote.”

15. Basi, mfalme akaja mto Yordani na watu wote wa Yuda wakaja mpaka Gilgali kumlaki mfalme na kumvusha mtoni Yordani.

16. Shimei mwana wa Gera, Mbenyamini, kutoka Bahurimu, alifanya haraka kwenda pamoja na watu wengine ili kumlaki mfalme Daudi.

17. Shimei alikwenda pamoja na Wabenyamini 1,000. Siba mtumishi wa jamaa ya Shauli, pamoja na watoto wake kumi na watumishi ishirini, walikwenda haraka mtoni Yordani kumtangulia mfalme Daudi.

18. Basi, wakavuka kwenye kivuko ili kuisindikiza jamaa ya mfalme na kumfanyia mfalme yote aliyoyapenda. Shimei mwana wa Gera akaja, akajitupa mbele ya mfalme, akasujudu, wakati mfalme alipokuwa karibu kuvuka mto Yordani.

19. Shimei akamwambia mfalme, “Nakuomba, bwana wangu mfalme, usinihesabu kuwa na hatia wala kukumbuka kosa nililofanya siku ile ulipokuwa ukiondoka mjini Yerusalemu. Nakuomba usiyaweke hayo maanani.

20. Maana, mimi mtumishi wako ninajua kwamba nilitenda dhambi. Hii ndiyo sababu nimekuja leo, nikiwa wa kwanza katika kabila la Yosefu, kuja kukulaki wewe bwana wangu, mfalme.”

21. Ndipo Abishai mwana wa Seruya akasema, “Je, si lazima Shimei auawe maana alimlaani mtu ambaye Mwenyezi-Mungu amemteua kwa kumpaka mafuta?”

22. Lakini Daudi akasema, “Wana wa Seruya, sina lolote nanyi; kwa nini mjifanye kama maadui zangu leo? Je, auawe mtu yeyote katika Israeli siku ya leo? Je, sijui kuwa mimi ni mfalme wa Israeli siku ya leo?”

23. Kisha, mfalme akamwambia Shimei, “Wewe hutauawa.” Mfalme akamwapia Shimei.

24. Mefiboshethi mjukuu wa Shauli, alikwenda pia kumlaki mfalme Daudi. Tangu siku ile mfalme alipoondoka Yerusalemu mpaka aliporudi salama, Mefiboshethi alikuwa hajapata kuosha miguu yake, kukata ndevu zake na hakujali kufua nguo zake.

25. Basi, ikawa alipofika Yerusalemu kumlaki mfalme, Daudi alimwuliza, “Je, Mefiboshethi, kwa nini hukuandamana pamoja nami?”

26. Mefiboshethi akasema, “Ee bwana wangu mfalme, mtumishi wangu alinidanganya. Maana, mimi mtumishi wako, nilimwambia, ‘Nitandikie punda nipate kumpanda kwenda pamoja na mfalme,’ maana mimi mtumishi wako ni kilema.

Kusoma sura kamili 2 Samueli 19