Agano la Kale

Agano Jipya

2 Samueli 13:17-37 Biblia Habari Njema (BHN)

17. Akamwita kijana wake aliyemtumikia, akamwambia, “Mtoe mwanamke huyu mbele yangu. Na mlango uufunge kwa komeo.”

18. Amnoni na yule kijana wakamtoa nje na kuufunga mlango kwa komeo. Tamari alikuwa amevaa vazi refu lenye mikono mirefu kwani hivyo ndivyo walivyovaa mabikira wa mfalme zamani hizo.

19. Basi, Tamari alijipaka majivu kichwani, akalipasua vazi lake, akaweka mikono yake kichwani, halafu akaondoka huku analia kwa sauti.

20. Kaka yake, Absalomu, alipomwona, alimwuliza, “Je, Amnoni kaka yako amelala nawe? Tulia dada yangu. Yeye ni kaka yako. Usilitie jambo hilo moyoni mwako.” Hivyo, Tamari aliishi katika nyumba ya Absalomu akiwa na huzuni na mpweke.

21. Mfalme Daudi aliposikia jambo hilo alikasirika sana.

22. Absalomu alimchukia Amnoni sana hata hakusema naye, kwa sababu alimshika kwa nguvu dada yake Tamari akalala naye.

23. Baada ya miaka miwili mizima, Absalomu alikuwa na shughuli ya kuwakata kondoo wake manyoya mjini Baal-hasori, karibu na Efraimu. Akawaalika watoto wote wa kiume wa mfalme.

24. Absalomu alimwendea mfalme Daudi, akamwambia, “Tazama, mimi mtumishi wako ninao wakata-kondoo manyoya. Nakuomba wewe mfalme pamoja na watumishi wako, mwende pamoja nami, mtumishi wako.”

25. Mfalme akamjibu, “Sivyo, mwanangu, tusiende wote; tusije tukawa mzigo kwako.” Ingawa Absalomu alizidi kumsihi baba yake aende, lakini mfalme alikataa, ila alimpa baraka zake.

26. Halafu, Absalomu akamwambia, “Kama huendi, basi, mruhusu ndugu yangu Amnoni twende naye.” Mfalme akamjibu, “Lakini kwa nini aende pamoja nanyi?”

27. Lakini Absalomu alizidi kumsihi, na mwishowe mfalme akamruhusu Amnoni na wanawe wengine waende kwenye sherehe hiyo.

28. Absalomu akawaambia watumishi wake, “Mwangalieni Amnoni atakapokuwa amekunywa divai na kufurahi. Nitakapowaambia, ‘Mpigeni Amnoni,’ muueni. Hiyo ni amri yangu kwenu. Jipeni moyo na muwe hodari.”

29. Hivyo, watumishi wa Absalomu walimtendea Amnoni kama walivyoamriwa na Absalomu, kisha wana wa kiume wengine wa mfalme wakaondoka kila mmoja akapanda nyumbu wake na kukimbia.

30. Walipokuwa bado njiani, Daudi alipata habari kuwa Absalomu amewaua watoto wake wote hakuna hata mmoja aliyesalia.

31. Mfalme Daudi aliinuka, akararua mavazi yake kwa huzuni akalala chini. Hata na watumishi wake wote waliokuwa wamesimama karibu naye walirarua mavazi yao.

32. Lakini Yonadabu, mwana wa Shimea, ndugu ya Daudi akamwambia, “Bwana wangu, usifikiri kuwa wanao wote wameuawa. Amnoni pekee ndiye aliyeuawa. Haya Absalomu aliyakusudia kuyafanya tangu wakati ule Amnoni alipomshika kwa nguvu dada yake Tamari na kulala naye.

33. Hivyo, bwana wangu, usifikiri moyoni mwako kwamba watoto wako wote wamekufa. Ni Amnoni pekee ndiye aliyeuawa.”

34. Lakini Absalomu alikuwa amekwisha kimbia. Naye kijana aliyekuwa na zamu ya ulinzi, mara akaona kundi kubwa la watu wanakuja kutokea mlimani katika barabara ya kutoka Horonaimu.

35. Yonadabu akamwambia Daudi, “Tazama mfalme, wanao wanakuja kama nilivyokuambia mimi mtumishi wako.”

36. Mara tu yule mtumishi alipomaliza kusema, wana wa kiume wa mfalme wakaingia, wakaanza kulia kwa sauti. Mfalme na watumishi wake wote, wakalia kwa uchungu.

37. Lakini Absalomu alikimbilia kwa Talmai mwana wa Amihudi, mfalme wa mji wa Geshuri. Mfalme Daudi akamwombolezea mwanawe Amnoni kwa siku nyingi.

Kusoma sura kamili 2 Samueli 13