Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wafalme 12:19-30 Biblia Habari Njema (BHN)

19. Hivyo watu wa Israeli wamekuwa katika hali ya uasi dhidi ya ukoo wa Daudi mpaka leo.

20. Watu wote wa Israeli walipopata habari kwamba Yeroboamu alikuwa amerudi kutoka Misri, walimwita katika mkutano wa hadhara, wakamtawaza kuwa mfalme wa Israeli yote. Hakuna kabila lingine lililojiunga na ukoo wa Daudi isipokuwa tu kabila la Yuda.

21. Rehoboamu alipofika Yerusalemu, alikusanya askari stadi 180,000 wa makabila ya Yuda na Benyamini, apate kupigana na utawala wa Israeli, ili aurudishe utawala kwake yeye mwenyewe Rehoboamu, mwana wa Solomoni.

22. Lakini ujumbe wa Mungu ulimjia Shemaya, mtu wa Mungu:

23. “Mwambie Rehoboamu mwana wa Solomoni, mfalme wa Yuda, na watu wote wa kabila la Yuda na Benyamini na watu wengine,

24. kwamba mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: ‘Msiende, wala msipigane na ndugu zenu, watu wa Israeli. Rudini kila mtu nyumbani kwake, maana hayo yaliyotokea ni mpango wangu.’” Basi, wakaufuata ujumbe huu wa Mwenyezi-Mungu, wakarudi nyumbani tena, kama Mwenyezi-Mungu alivyoagiza.

25. Baadaye mfalme Yeroboamu akaujenga upya mji wa Shekemu kwenye mlima wa Efraimu; akakaa huko. Kisha akaenda akajenga mji wa Penueli.

26. Ndipo Yeroboamu akaanza kufikirifikiri: “Sasa ufalme utarudi kwa jamaa ya mfalme Daudi

27. kama watu hawa wataendelea kwenda kutambikia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu huko Yerusalemu. Mioyo yao itamgeukia bwana wao Rehoboamu mfalme wa Yuda, nao wataniua mimi.”

28. Basi, baada ya kushauriana na wengine, akatengeneza sanamu za ndama mbili za dhahabu. Kisha akawaambia watu, “Enyi watu wa Israeli, hii ndiyo miungu yenu iliyowatoa katika nchi ya Misri! Hakuna sababu ya kwenda Yerusalemu kutambikia huko.”

29. Akaweka sanamu moja ya ndama wa dhahabu mjini Betheli, na ya pili mjini Dani.

30. Tendo hili likawa dhambi, maana watu waliandamana kwenda kuzitambikia sanamu hizo huko Betheli na Dani.

Kusoma sura kamili 1 Wafalme 12