Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wafalme 12:1-17 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Basi, Rehoboamu akaenda Shekemu ambako Waisraeli wote walikuwa wamekusanyika ili kumtawaza awe mfalme.

2. Naye Yeroboamu mwana wa Nebati alipopata habari kuhusu tendo hilo (maana alikuwa bado Misri ambako alikwenda alipomkimbia Solomoni), alirudi kutoka Misri.

3. Lakini Waisraeli walituma ujumbe na kumwita. Kisha, yeye pamoja na jumuiya yote ya Israeli, walimwendea Rehoboamu, wakamwambia,

4. “Baba yako alitutwisha mzigo mzito. Basi, utupunguzie mzigo huo, nasi tutakutumikia.”

5. Naye Rehoboamu akawaambia, “Nendeni, mrudi kwangu kesho kutwa.” Basi, wakaondoka.

6. Baadaye Rehoboamu alitaka kujua maoni ya wazee ambao walikuwa washauri wa baba yake Solomoni, alipokuwa angali hai, akawauliza, “Je, mnanishauri niwape jibu gani watu hawa?”

7. Wazee hao wakamjibu, “Leo ukiwa mtumishi wa watu hawa, ukawatumikia na kuongea nao vizuri unapowajibu, hapo watakuwa watumishi wako daima.”

8. Lakini Rehoboamu alipuuza shauri la wazee; badala yake akashauriana na vijana wa rika lake ambao walikuwa washauri wake.

9. Basi, akawauliza, “Nyinyi mnatoa shauri gani ili tuweze kuwajibu watu hawa walioniambia niwapunguzie mzigo ambao baba yangu aliwatwika?”

10. Hao vijana wakamjibu, “Watu hao waliokuambia baba yako aliwatwika mzigo mzito, wakakuomba uwapunguzie mzigo huo, wewe waambie hivi: ‘Kidole changu kidogo ni kinene zaidi kuliko kiuno cha baba yangu.

11. Mzigo wa baba yangu ulikuwa mzito, lakini wangu utakuwa mzito zaidi. Baba yangu aliwapiga kwa mijeledi, lakini mimi nitawapiga kwa mijeledi yenye miiba.’”

12. Basi, siku ya tatu Yeroboamu pamoja na watu wote wakarudi kwa Rehoboamu kama alivyokuwa amewaagiza.

13. Mfalme akawajibu watu hao kwa ukali, akapuuza shauri alilopewa na wazee,

14. akafuata shauri la vijana wenzake, akawaambia, “Baba yangu aliwatwika mzigo mzito, lakini mimi nitaufanya kuwa mzito zaidi. Baba yangu aliwapiga kwa mijeledi, lakini mimi nitawapiga kwa mijeledi yenye miiba.”

15. Hivyo, mfalme hakuwajali watu kwa sababu jambo hili lilisababishwa na Mwenyezi-Mungu, ili atimize neno lake alilomwambia Yeroboamu mwana wa Nebati, kwa njia ya Ahiya wa Shilo.

16. Lakini watu wote wa Israeli walipoona kwamba mfalme hakuwajali, walimwambia,“Hatuna uhusiano wowote na Daudi!Hatuna sehemu yetu kutoka kwa huyo mwana wa Yese.Rudini nyumbani, enyi watu wa Israeli!Itunze nyumba yako mwenyewe, ee Daudi.”Hivyo, watu wa Israeli wakarudi makwao.

17. Watu wa Israeli waliokuwa wanakaa katika miji ya Yuda, ndio hao tu waliobaki chini ya utawala wa Rehoboamu.

Kusoma sura kamili 1 Wafalme 12