Agano la Kale

Agano Jipya

1 Samueli 3:3-13 Biblia Habari Njema (BHN)

3. Samueli naye alikuwa amelala ndani ya hekalu la Mwenyezi-Mungu karibu na sanduku la agano la Mungu. Taa ya Mwenyezi-Mungu ilikuwa bado inawaka kwani kulikuwa hakujapambazuka.

4. Ndipo Mwenyezi-Mungu akamwita Samueli! Naye Samueli, akaitika, “Naam!”

5. Kisha Samueli akamwendea Eli kwa haraka, akamwambia, “Nimekuja kwani umeniita.” Lakini Eli akamwambia, “Mimi sijakuita. Nenda ukalale.” Samueli akarudi na kulala.

6. Mwenyezi-Mungu akamwita tena, “Samueli!” Samueli akaamka, akamwendea Eli na kumwambia, “Nimekuja, kwani umeniita.” Lakini Eli akamwambia, “Sikukuita mwanangu, kalale tena.”

7. Samueli alikuwa hamjui Mwenyezi-Mungu bado, wala ujumbe wa Mwenyezi-Mungu ulikuwa bado haujafunuliwa kwake.

8. Mwenyezi-Mungu akamwita Samueli kwa mara ya tatu. Samueli akaamka, akamwendea Eli na kumwambia, “Nimekuja, kwani umeniita.” Ndipo Eli alipotambua kuwa Mwenyezi-Mungu ndiye aliyemwita Samueli.

9. Kwa hiyo Eli akamwambia Samueli, “Nenda ukalale, na akikuita, mwambie hivi: ‘Sema, ee Mwenyezi-Mungu, kwani mimi mtumishi wako nasikiliza.’” Hivyo Samueli akarudi na kulala mahali pake.

10. Baadaye Mwenyezi-Mungu akaja na kusimama hapo, akamwita Samueli kama hapo awali, “Samueli! Samueli!” Samueli akasema, “Sema, kwani mimi mtumishi wako nasikiliza.”

11. Kisha, Mwenyezi-Mungu akamwambia Samueli, “Tazama, nataka kutenda jambo fulani katika Israeli ambalo kila atakayesikia, atashtuka kulisikia.

12. Siku hiyo, nitatimiza yale yote niliyosema tangu mwanzo hadi mwisho dhidi ya Eli kuhusu jamaa yake.

13. Nimekwisha mwambia kuwa nitaiadhibu jamaa yake milele, kwa uovu anaoujua kwa sababu watoto wake wa kiume wamenikufuru mimi na hakuwazuia.

Kusoma sura kamili 1 Samueli 3