Agano la Kale

Agano Jipya

1 Samueli 16:8-22 Biblia Habari Njema (BHN)

8. Kisha, Yese akamwita Abinadabu na kumleta mbele ya Samueli. Lakini Samueli akasema, “Wala huyu hakuchaguliwa na Mwenyezi-Mungu.”

9. Yese akamleta Shama. Samueli akasema, “Wala huyu hakuchaguliwa na Mwenyezi-Mungu.”

10. Yese aliwapitisha wanawe wote saba mbele ya Samueli lakini Samueli akamwambia, “Mwenyezi-Mungu hajamchagua yeyote kati ya hawa.”

11. Halafu akamwambia, “Je, wanao wote wako hapa?”Yese akajibu, “Bado yuko mdogo, lakini amekwenda kuchunga kondoo.” Samueli akamwambia, “Mtume mtu amlete; sisi hatutaketi chini, mpaka atakapokuja hapa.”

12. Hivyo, Yese alituma mtu, naye akaletwa. Yule kijana alikuwa mwenye afya, mwenye macho maangavu na wa kupendeza. Mwenyezi-Mungu akamwambia Samueli, “Sasa, huyu ndiye; inuka umpake mafuta.”

13. Samueli akachukua upembe wake wenye mafuta akammiminia Daudi mafuta mbele ya kaka zake. Mara roho ya Mwenyezi-Mungu ikamjia Daudi kwa nguvu, ikakaa tangu siku hiyo na kuendelea. Kisha Samueli akarudi mjini Rama.

14. Baadaye roho ya Mwenyezi-Mungu ilimwacha Shauli, na roho mwovu kutoka kwa Mwenyezi-Mungu ikamsumbua.

15. Ndipo watumishi wake Shauli wakamwambia, “Tunajua kwamba roho mwovu kutoka kwa Mungu anakusumbua.

16. Sasa, ee bwana wetu, amuru watumishi wako wanaokutumikia wamtafute mtu mwenye ufundi wa kupiga kinubi, na huyo roho mwovu kutoka kwa Mungu atakapokujia, mtu huyo atapiga kinubi, nawe utapata nafuu.”

17. Shauli akawaambia watumishi wake, “Nitafutieni mtu huyo anayeweza kupiga kinubi vizuri, mniletee.”

18. Kijana mmoja miongoni mwa watumishi akasema, “Nimemwona kijana mmoja wa Yese, wa mji wa Bethlehemu. Kijana huyo ana ujuzi wa kupiga kinubi. Huyo kijana ni shujaa, hodari wa kupigana vitani, ana busara katika kusema na mwenye umbo zuri; Mwenyezi-Mungu yuko pamoja naye.”

19. Hivyo, Shauli alituma ujumbe kwa Yese, na kusema, “Nitumie mwanao Daudi, ambaye anachunga kondoo.”

20. Yese alimtuma Daudi kwa Shauli pamoja na punda aliyebeba mikate, kiriba cha divai na mwanambuzi.

21. Daudi alipofika akaingia kumtumikia Shauli. Shauli alimpenda sana, hata akamfanya awe mwenye kumbebea silaha zake.

22. Halafu Shauli alituma ujumbe kwa Yese na kusema, “Nampenda Daudi; mwache akae hapa anitumikie.”

Kusoma sura kamili 1 Samueli 16