Agano la Kale

Agano Jipya

Yeremia 44:18-29 Biblia Habari Njema (BHN)

18. Lakini tangu tuache kumfukizia ubani malkia wa mbinguni na kummiminia kinywaji, tumetindikiwa kila kitu, na tumeangamizwa kwa vita na njaa.”

19. Nao wanawake wakasema, “Tulimfukizia ubani na kummiminia kinywaji malkia wa mbinguni. Tulifanya hivyo kwa kibali cha waume zetu. Tena tulimtengenezea mikate yenye sura yake na kummiminia kinywaji!”

20. Ndipo Yeremia akawaambia watu wote, wanaume kwa wanawake, yaani watu wote waliompa jibu hilo:

21. “Kuhusu matambiko ambayo nyinyi na wazee wenu, wafalme wenu na viongozi wenu, pamoja na wananchi wote, mlifanya katika miji ya Yuda na katika barabara za Yerusalemu, je, mnadhani Mwenyezi-Mungu amesahau au hakumbuki?

22. Mwenyezi-Mungu hakuweza kuvumilia tena matendo yenu maovu na mambo ya kuchukiza mliyotenda; ndiyo maana nchi yenu imekuwa ukiwa, jangwa, laana na bila wakazi, kama ilivyo mpaka leo.

23. Maafa haya yamewapata mpaka leo kwa sababu mliitolea sadaka za kuteketezwa miungu mingine na kumkosea Mwenyezi-Mungu, mkakataa kutii sauti yake au kufuata sheria yake, kanuni zake na maagizo yake.”

24. Yeremia aliwaambia watu wote na wanawake wote: “Sikilizeni neno la Mwenyezi-Mungu, enyi watu wa Yuda wote mlioko nchini Misri.

25. Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi: Nyinyi pamoja na wake zenu mmetekeleza kwa vitendo yale mliyotamka kwa vinywa vyenu, mkisema kwamba mmepania kutimiza viapo vyenu mlivyofanya vya kumtolea sadaka na kummiminia kinywaji malkia wa mbinguni. Haya basi! Shikeni viapo vyenu na kutoa sadaka za vinywaji!

26. Lakini sikilizeni neno langu mimi Mwenyezi-Mungu, enyi watu wote wa Yuda mnaokaa nchini Misri. Mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Naapa kwa jina langu kuu kwamba hakuna mtu yeyote wa Yuda katika nchi yote ya Misri atakayelitumia jina langu kuapa nalo akisema: ‘Kama aishivyo Bwana Mwenyezi-Mungu!’

27. Mimi nawachungulia hao sio kwa mema bali kwa mabaya. Watu wote wa Yuda nchini Misri wataangamizwa kwa upanga na njaa, asibaki hata mtu mmoja.

28. Ni wachache watakaonusurika vitani na kurudi kutoka nchi ya Misri na kwenda nchini Yuda. Hapo watu wa Yuda wote waliobaki kati ya wale waliokwenda kukaa Misri watatambua ni tamko la nani lenye nguvu: Langu au lao!

29. Mimi Mwenyezi-Mungu nasema kwamba nitawaadhibu hapahapa mpate kujua kwamba maneno ya maafa niliyotamka dhidi yenu yatatimia. Na hii itakuwa ishara yake:

Kusoma sura kamili Yeremia 44