Agano la Kale

Agano Jipya

Yeremia 36:14-25 Biblia Habari Njema (BHN)

14. Kisha, wakuu walimtuma Yehudi mwana wa Nethania, mjukuu wa Shelemia, kitukuu cha Kushi, amwambie Baruku hivi: “Chukua ile hati ya maandishi uliyosoma mbele ya watu uje nayo hapa.” Basi, Baruku mwana wa Neria, akachukua hati mkononi mwake, akawaendea.

15. Nao wakamwambia: “Keti, uisome.” Baruku akawasomea.

16. Waliposikia maneno hayo yote, walitazamana kwa hofu. Wakamwambia Baruku, “Hatuna budi kumweleza mfalme maneno haya yote.”

17. Kisha wakamwuliza Baruku, “Hebu tuambie, umepataje kuandika maneno yote haya? Je, Yeremia alisema, nawe ukayaandika?”

18. Baruku akawajibu: “Yeye alisema, nami nikawa nayaandika kwa wino katika hati hii.”

19. Kisha wakuu hao wakamwambia Baruku, “Wewe nenda ukajifiche pamoja na Yeremia, na pasiwe na mtu yeyote atakayejua mahali mlipo.”

20. Baada ya wakuu kuweka hati ile ndefu katika chumba cha Elishama katibu wa mfalme, walimwendea mfalme ukumbini, wakamjulisha mambo yote.

21. Kisha, mfalme alimtuma Yehudi aende kuleta ile hati. Yehudi aliichukua kutoka chumbani mwa katibu Elishama, akamsomea mfalme na wakuu wote waliokuwa wamesimama karibu na mfalme.

22. Wakati huo ulikuwa mwezi wa tisa, na mfalme alikuwa ndani ya nyumba yake ya majira ya baridi, akiota moto wa makaa.

23. Ikawa, mara baada ya Yehudi kusoma safu tatu au nne hivi za hiyo hati ndefu, mfalme alizikata safu hizo kwa kisu na kuzitupa katika moto wa makaa. Aliendelea kufanya hivyo mpaka hati yote ikateketea.

24. Lakini, ingawa mfalme na watumishi wake wote waliyasikia maneno hayo yote, hawakuogopa wala kuyararua mavazi yao kwa huzuni.

25. Ijapokuwa Elnata, Delaya na Gemaria walimsihi mfalme asiichome hati hiyo, mfalme hakuwasikiliza.

Kusoma sura kamili Yeremia 36