Agano la Kale

Agano Jipya

Waamuzi 19:6-23 Biblia Habari Njema (BHN)

6. Basi hao watu wawili wakakaa, wakala na kunywa pamoja. Kisha baba mkwe wake akamwambia, “Tafadhali ulale hapa usiku huu na kufurahi.”

7. Yule mtu aliposimama akitaka kuondoka, baba mkwe wake akamhimiza abaki, naye akabaki.

8. Siku ya tano huyo mtu aliamka asubuhi, akitaka kuondoka. Lakini baba yake yule mwanamke akamwambia, “Kwanza upate nguvu kwa kula, ungoje alasiri, halafu uondoke.” Basi wote wawili wakala pamoja.

9. Huyo Mlawi na suria wake pamoja na mtumishi wake walipoinuka kwenda zao, baba mkwe wake akamwambia huyo Mlawi, “Sasa mchana umekwisha na jioni imekaribia. Ulale hapa, na kufurahi. Kesho asubuhi utaamka mapema kuanza safari yako ya kurudi nyumbani.”

10. Lakini huyo mtu alikataa kulala huko usiku huo. Basi, akainuka, akaondoka akafika karibu na mji wa Yebusi (yaani Yerusalemu). Alikuwa na wale punda wake wawili waliotandikwa tayari, pamoja na suria wake.

11. Walipokuwa wamekaribia mjini Yebusi, siku ilikuwa karibu imekwisha; naye mtumishi akamwambia bwana wake, “Sasa heri tuingie katika mji huu wa Wayebusi tulale humo usiku huu.”

12. Bwana wake akamjibu, “Hatutageuka na kuingia katika mji wa wageni ambao si Waisraeli. Tutaendelea na safari mpaka Gibea.

13. Twende tukaribie sehemu hizo na kulala huko Gibea au Rama.”

14. Basi, wakaendelea na safari yao mpaka jua likatua wakiwa karibu na mji wa Gibea ambao ni mji wa kabila la Benyamini.

15. Wakaingia mjini wapate kulala humo usiku. Walipoingia mjini wakaenda kukaa kwenye uwanja wa wazi wa mji, kwani hakuna mtu aliyewakaribisha nyumbani kwake.

16. Walipokuwa huko mzee mmoja akafika kutoka shambani kwake. Mzee huyo alikuwa mwenyeji wa nchi ya milima ya Efraimu na alikuwa akiishi huko Gibea kama mgeni. Wakazi wa mji wa Gibea walikuwa wa kabila la Benyamini.

17. Mzee huyo alipotazama na kumwona huyo msafiri akiwa huko uwanjani, alimwuliza, “Umetoka wapi na unakwenda wapi?”

18. Naye akamjibu, “Tumetoka Bethlehemu nchini Yuda na tunaelekea sehemu za mbali za eneo la milima ya Efraimu. Huko ndiko ninakoishi na sasa ninarudi safarini huko Bethlehemu katika Yuda na kurejea nyumbani; hakuna mtu hapa aliyetukaribisha nyumbani kwake.

19. Lakini sisi watumishi wako tuna nyasi na malisho kwa ajili ya punda wetu. Pia nina mkate na divai; hivyo vinanitosha mimi, suria wangu na mtumishi wangu. Hatupungukiwi kitu chochote.”

20. Huyo mzee akamwambia, “Amani iwe nanyi! Nitawapa mahitaji yote. Ila msilale huku uwanjani.”

21. Hivyo akawapeleka nyumbani kwake na kuwapa punda wao malisho. Hao wasafiri wakanawa miguu yao, wakala na kunywa.

22. Walipokuwa wanajifurahisha, kumbe wanaume mabaradhuli wa mji huo wakaja wakaizingira hiyo nyumba na kugonga mlangoni. Wakamwambia mzee mwenye nyumba, “Mtoe nje yule mwanamume aliyekuja kwako, tulale naye.”

23. Lakini huyo mzee mwenye nyumba akatoka nje, akawaambia “Sivyo ndugu zangu; nawasihi msitende uovu huo. Huyu ni mgeni wangu, hivyo msimtendee ubaya huo.

Kusoma sura kamili Waamuzi 19