Agano la Kale

Agano Jipya

Waamuzi 15:3-16 Biblia Habari Njema (BHN)

3. Samsoni akamwambia, “Safari hii sitakuwa na lawama kwa yale nitakayowatendea Wafilisti.”

4. Basi, Samsoni akaenda, akawakamata mbweha 300 na akawafunga mikia yao pamoja wawiliwawili. Kisha akaweka mwenge katika kila jozi ya mbweha.

5. Halafu akaiwasha hiyo mienge na kuwaachilia hao mbweha ambao waliingia kwenye mashamba ya Wafilisti na kuteketeza miganda ya ngano na pia ngano iliyokuwa bado haijavunwa hata na mashamba ya mizeituni.

6. Wafilisti walipotaka kujua aliyefanya hayo, waliambiwa, “Ni huyo Samsoni, mkwewe Mtimna, amefanya hivyo kwa sababu huyo baba mkwe wake amemchukua mke wake na kumwoza kwa kijana mmoja aliyekuwa mdhamini wake mwenyewe Samsoni katika harusi.” Basi Wafilisti wakaenda kumchoma moto yule mwanamke pamoja na baba yake.

7. Samsoni akawaambia hao Wafilisti, “Kama hayo ndiyo mliyoyafanya, naapa kwamba sitaondoka mpaka nimelipiza kisasi.”

8. Basi, akawashambulia vikali na kuwaua wengi. Kisha akaenda kuishi katika pango la mwamba wa Etamu.

9. Wafilisti wakaja, wakapiga kambi yao nchini Yuda na kuushambulia mji wa Lehi.

10. Watu wa Yuda wakawauliza, “Kwa nini mmekuja kutushambulia?” Nao wakawajibu, “Tumekuja ili tumfunge Samsoni na kumtendea kama alivyotutendea.”

11. Basi, watu 3,000 wa Yuda wakamwendea Samsoni pangoni mwa mwamba wa Etamu wakamwambia, “Je, hujui kwamba Wafilisti wanatawala juu yetu? Tazama basi, mkosi uliotutendea!” Samsoni akawajibu, “Kama walivyonitendea ndivyo nilivyowatendea.”

12. Wakamwambia, “Tumekuja kukufunga ili tukutie mikononi mwao.” Samsoni akawaambia, “Niapieni kwamba nyinyi wenyewe hamtaniua.”

13. Nao wakamwambia, “Sisi hatutakuua ila tutakufunga tu na kukutia mikononi mwao.” Basi, wakamfunga kwa kamba mbili mpya na kumtoa humo pangoni.

14. Alipofika Lehi, Wafilisti walimwendea mbio huku wakipiga kelele. Ghafla roho ya Mwenyezi-Mungu ikamjia Samsoni kwa nguvu na zile kamba walizomfunga mikononi mwake zikakatika kama kitani kilichoshika moto, navyo vifungo vikaanguka chini.

15. Samsoni akapata utaya mbichi wa punda, akautumia kuwaua watu 1,000.

16. Kisha Samsoni akasema,“Kwa utaya wa punda,nimeua watu elfu moja.Kwa utaya wa punda,nimekusanya marundo ya maiti.”

Kusoma sura kamili Waamuzi 15