Agano la Kale

Agano Jipya

Malaki 2:6-15 Biblia Habari Njema (BHN)

6. Mafundisho yao yalikuwa ya kweli na kamwe hawakufundisha uongo. Mimi na wao tulikaa kwa amani. Si kwamba walitenda haki tu, bali waliwafundisha wengine kutotenda maovu.

7. Ni wajibu wa makuhani kuwafundisha watu maarifa ya kweli juu ya Mungu. Watu wawaendee kujifunza matakwa yangu kwao, kwani makuhani ni wajumbe wa Mwenyezi-Mungu wa majeshi.

8. “Bali nyinyi makuhani mmegeuka mkaiacha njia ya haki. Mafundisho yenu yamewaongoza watu wengi katika kutenda mabaya. Mmelivunja agano nililofanya nanyi.

9. Nami pia nitawafanya mdharauliwe na kupuuzwa na Waisraeli, kwa sababu hamkuzifuata njia zangu, na mnapowafundisha watu wangu mnapendelea baadhi yao.”

10. Je, sisi sote si watoto wa baba mmoja? Je, sisi sote hatukuumbwa na Mungu yuleyule? Mbona basi, hatuaminiani sisi kwa sisi, na tunalidharau agano alilofanya Mwenyezi-Mungu na wazee wetu?

11. Watu wa Yuda wamekosa uaminifu kwa Mungu na kutenda machukizo katika Israeli na mjini Yerusalemu. Wamelitia unajisi hekalu la Mwenyezi-Mungu analolipenda. Tena wameoa wanawake wanaoabudu miungu ya kigeni.

12. Mwenyezi-Mungu na awaondolee mbali watu wanaofanya mambo hayo kutoka miongoni mwa wazawa wa Yakobo. Na kamwe wasishiriki katika kutoa ushuhuda na kuleta tambiko mbele ya Mwenyezi-Mungu wa majeshi.

13. Zaidi ya hayo yote, mnaifunika madhabahu ya Mwenyezi-Mungu kwa machozi yenu, mkilia na kuomboleza kwa sababu yeye hazikubali tena tambiko mnazomtolea.

14. Mnauliza, “Mbona sasa hazikubali?” Mwenyezi-Mungu hazikubali kwa sababu anajua wazi kuwa umeivunja ahadi yako kwa mke wa ujana wako. Umekosa uaminifu kwake ingawa uliahidi mbele ya Mungu kwamba ungekuwa mwaminifu kwake.

15. Je, Mungu hakuwafanya nyote wawili muwe mwili mmoja na roho moja? Je, alikusudia nini alipofanya hayo? Yamkini alikusudia tuzae watoto ambao watamcha yeye. Kwa hiyo, hakikisheni kuwa hakuna hata mmoja wenu anayekosa uaminifu kwa mkewe.

Kusoma sura kamili Malaki 2