Agano la Kale

Agano Jipya

Ezekieli 34:5-16 Biblia Habari Njema (BHN)

5. Basi, kwa kuwa hao kondoo hawakuwa na mchungaji walitawanywa, wakawa mawindo ya wanyama wakali.

6. Naam, kondoo wangu walitawanywa, wakatangatanga milimani na vilimani. Kondoo walisambazwa duniani kote, na hapakuwa na mtu aliyejali juu yao wala kuwatafuta.

7. “Basi, sikieni vizuri neno langu mimi Mwenyezi-Mungu, enyi wachungaji:

8. Kama niishivyo mimi Bwana Mwenyezi-Mungu, naapa kwamba: Nimechoka kuwaona kondoo wangu wamekuwa mawindo ya wanyama wakali kwa vile hapakuwa na mchungaji; wachungaji wangu hawakuwatafuta kondoo wangu, bali wamejilisha wao wenyewe badala ya kuwalisha kondoo wangu.

9. Basi, nyinyi wachungaji, sikieni neno langu mimi Mwenyezi-Mungu.

10. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitapambana nanyi, enyi wachungaji. Nitawaondolea madaraka ya kuchunga kondoo wangu, wala sitakubali muwachunge tena. Hamtakuwa tena na nafasi ya kujinufaisha wenyewe. Nitawaokoa kondoo wangu makuchani mwenu, ili wasiwe chakula chenu tena.

11. “Basi, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Mimi mwenyewe nitawatafuta kondoo wangu na kuwatunza.

12. Kama mchungaji anavyowatafuta kondoo wake waliotawanyika, ndivyo nitakavyowatafuta kondoo wangu. Nitawarudisha kutoka kila mahali walipotawanyika siku yenye mawingu na giza nene.

13. Nitawatoa kutoka kwa watu wa mataifa. Nitawakusanya kutoka nchi za mbali na kuwaleta katika nchi yao wenyewe. Nitawachunga juu ya milima ya Israeli, kando ya vijito na katika sehemu zote za nchi zinazokaliwa na watu.

14. Nitawapa malisho mazuri kwenye milima mirefu ya Israeli ambako yako malisho yao. Watapumzika huko kwenye mbuga za malisho mazuri; naam, watapata malisho mazuri juu ya milima ya Israeli.

15. Mimi mwenyewe nitakuwa mchungaji wa kondoo wangu. Mimi mwenyewe nitawapumzisha. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.

16. Kondoo waliopotea nitawatafuta na waliotangatanga nitawarudisha nyumbani. Waliojeruhiwa nitawatibu, na wale walio dhaifu nitawapa nguvu. Kondoo wanono na wenye nguvu nitawaangamiza. Mimi nitawachunga kondoo kama itakiwavyo.

Kusoma sura kamili Ezekieli 34