Agano la Kale

Agano Jipya

Ezekieli 34:3-13 Biblia Habari Njema (BHN)

3. Mnakunywa maziwa, mnavaa mavazi ya manyoya yao na kondoo wanono mnawachinja na kuwala. Lakini hamwalishi hao kondoo.

4. Walio dhaifu hamkuwapatia nguvu, wagonjwa hamkuwaponya, waliojeruhiwa hamkuwafungia dawa, waliotangatanga hamkuwarudisha na waliopotea hamkuwatafuta. Lakini mmetumia mabavu na ukatili kuwatawala.

5. Basi, kwa kuwa hao kondoo hawakuwa na mchungaji walitawanywa, wakawa mawindo ya wanyama wakali.

6. Naam, kondoo wangu walitawanywa, wakatangatanga milimani na vilimani. Kondoo walisambazwa duniani kote, na hapakuwa na mtu aliyejali juu yao wala kuwatafuta.

7. “Basi, sikieni vizuri neno langu mimi Mwenyezi-Mungu, enyi wachungaji:

8. Kama niishivyo mimi Bwana Mwenyezi-Mungu, naapa kwamba: Nimechoka kuwaona kondoo wangu wamekuwa mawindo ya wanyama wakali kwa vile hapakuwa na mchungaji; wachungaji wangu hawakuwatafuta kondoo wangu, bali wamejilisha wao wenyewe badala ya kuwalisha kondoo wangu.

9. Basi, nyinyi wachungaji, sikieni neno langu mimi Mwenyezi-Mungu.

10. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitapambana nanyi, enyi wachungaji. Nitawaondolea madaraka ya kuchunga kondoo wangu, wala sitakubali muwachunge tena. Hamtakuwa tena na nafasi ya kujinufaisha wenyewe. Nitawaokoa kondoo wangu makuchani mwenu, ili wasiwe chakula chenu tena.

11. “Basi, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Mimi mwenyewe nitawatafuta kondoo wangu na kuwatunza.

12. Kama mchungaji anavyowatafuta kondoo wake waliotawanyika, ndivyo nitakavyowatafuta kondoo wangu. Nitawarudisha kutoka kila mahali walipotawanyika siku yenye mawingu na giza nene.

13. Nitawatoa kutoka kwa watu wa mataifa. Nitawakusanya kutoka nchi za mbali na kuwaleta katika nchi yao wenyewe. Nitawachunga juu ya milima ya Israeli, kando ya vijito na katika sehemu zote za nchi zinazokaliwa na watu.

Kusoma sura kamili Ezekieli 34