Agano la Kale

Agano Jipya

Danieli 2:35-46 Biblia Habari Njema (BHN)

35. Mara kile chuma, udongo wa mfinyanzi, shaba, fedha na dhahabu, vyote vikavunjika vipandevipande na kuwa kama makapi ya mahali pa kupuria nafaka wakati wa kiangazi. Upepo ukavipeperushia mbali kisibakie hata kipande kimoja. Lakini lile jiwe lililoivunja ile sanamu likageuka kuwa mlima mkubwa na kuijaza dunia yote.

36. “Hiyo ndiyo ndoto yako, ee mfalme. Na sasa tutakupa maana yake.

37. Wewe, ee mfalme, mfalme wa wafalme! Mungu amekupa ufalme, uwezo, nguvu na utukufu!

38. Amekupa mamlaka juu ya wanaadamu wote, wanyama wa porini na ndege wote wa angani, kokote kule waliko. Wewe ndiwe kile kichwa cha dhahabu!

39. Baada yako utafuata ufalme mwingine, lakini ufalme huo utakuwa dhaifu. Huu utafuatwa na ufalme wa tatu unaofananishwa na shaba; huo utaitawala dunia yote.

40. Baada ya falme hizo, utafuata ufalme mwingine imara kama chuma. Na kama vile chuma kivunjavyo na kupondaponda vitu vyote, ndivyo ufalme huo utakavyovunjavunja na kusagilia mbali falme zilizotangulia.

41. Uliona pia kuwa nyayo na vidole vya sanamu hiyo vilikuwa nusu udongo wa mfinyanzi na nusu chuma. Hii ina maana kwamba ufalme huo utagawanyika; lakini utakuwa na kiasi fulani cha nguvu za chuma kwa sababu kulikuwa na chuma kilichochanganyikana na udongo wa mfinyanzi.

42. Kama ulivyoona, vidole vyake vya miguu vilikuwa nusu chuma na nusu udongo wa mfinyanzi, na hii inamaanisha kwamba ufalme huo utakuwa na nguvu kiasi fulani na udhaifu kiasi fulani.

43. Hii inamaanisha kwamba watawala wa ufalme huo watachanganyikana kwa kuoana na watu wasio wa taifa lao, lakini hawatafaulu kuchanganyikana kama vile chuma kisivyoweza kuchanganyikana na udongo wa mfinyanzi.

44. Wakati wa wafalme hao, Mungu wa mbinguni ataanzisha ufalme ambao kamwe hautaangamizwa. Watu wengine hawataushinda na kuutawala ufalme huo, bali ufalme huo utaziponda na kuzikomesha falme zilizotangulia, nao utadumu milele.

45. Uliliona jiwe lililongoka lenyewe toka mlimani, bila kuguswa, na jinsi lilivyoivunja vipandevipande ile sanamu iliyotengenezwa kwa chuma, shaba, udongo wa mfinyanzi, fedha na dhahabu. Ee mfalme, Mungu Mkuu amekufunulia mambo yatakayotukia baadaye. Mimi nimekusimulia. Ndoto yako ni ya kweli na maana yake ni halisi.”

46. Ndipo mfalme Nebukadneza alipoanguka kifudifudi na kumsujudia Danieli na kuamuru wamtolee Danieli tambiko na ubani.

Kusoma sura kamili Danieli 2