Agano la Kale

Agano Jipya

2 Wafalme 9:22-30 Biblia Habari Njema (BHN)

22. Ikawa Yoramu, alipomwona Yehu, alimwuliza, “Je, kuna amani, Yehu?” Yehu akamjibu, “Amani gani, wakati makahaba na wachawi wa Yezebeli ni wengi?”

23. Yoramu aligeuza gari lake na kuondoka, huku akimwambia Ahazia, “Huu ni uhaini Ahazia!”

24. Yehu akatwaa upinde wake na kutupa mshale ambao ulipenya mabega ya Yoramu na kuchoma moyo wake, naye akafa papo hapo garini mwake.

25. Yehu akamwambia msaidizi wake Bidkari, “Chukua hiyo maiti yake uitupe katika shamba hilo la Nabothi Myezreeli. Kwa maana, kumbuka wewe na mimi tulipokuwa tumepanda farasi wetu nyuma ya baba yake Ahabu, jinsi Mwenyezi-Mungu alivyonena maneno haya dhidi yake.

26. Mwenyezi-Mungu alisema, ‘Kwa ile damu ya Nabothi na kwa damu ya wanawe niliyoona jana naapa kwamba nitakulipiza kisasi katika shamba hilo.’ Kwa hiyo, chukua maiti ya Yoramu uitupe katika shamba la Nabothi kama alivyosema Mwenyezi-Mungu.”

27. Ahazia mfalme wa Yuda alipoona yaliyotukia alikimbia akielekea Nyumba ya Bustani, huku akifuatwa na Yehu. Yehu akawaamuru watu wake, “Muueni naye pia!” Nao wakampiga mshale akiwa garini kwenye njia ya kupanda Guri karibu na mji wa Ibleamu. Halafu alikimbilia Megido na kufia huko.

28. Maofisa wake wakaichukua maiti yake ndani ya gari lake na kuipeleka Yerusalemu; na huko akazikwa katika makaburi ya kifalme katika mji wa Daudi.

29. Ahazia alianza kutawala juu ya Yuda katika mwaka wa kumi na moja wa enzi ya Yoramu mwana wa Ahabu.

30. Yehu alipofika Yezreeli, Yezebeli alikuwa amekwisha pata habari za mambo yaliyotokea. Alijipaka rangi machoni na kupanga nywele zake, ndipo akaenda dirishani na kuangalia chini.

Kusoma sura kamili 2 Wafalme 9