Agano la Kale

Agano Jipya

2 Wafalme 8:2-17 Biblia Habari Njema (BHN)

2. Huyo mwanamke akaondoka akafanya kama mtu wa Mungu alivyosema akaenda pamoja na jamaa yake na kukaa kama mgeni katika nchi ya Filistia kwa miaka saba.

3. Miaka saba ilipokwisha, alitoka Filistia akarudi Israeli na kwenda kwa mfalme kuomba arudishiwe nyumba yake na shamba lake.

4. Akamkuta mfalme anaongea na Gehazi, akisema, “Tafadhali nieleze miujiza ambayo hutendwa na Elisha.”

5. Gehazi alipokuwa anamweleza mfalme jinsi Elisha alivyofufua mtu aliyekufa, mwanamke huyo alitoa ombi lake kwa mfalme. Gehazi akasema, “Ee mfalme; huyu ndiye mwanamke ambaye Elisha alimfufua mwanawe!”

6. Mfalme alipomwuliza mwanamke huyo, yeye alimweleza. Mfalme akamwita ofisa wake na kumwamuru amrudishie mwanamke huyo mali yake yote, pamoja na mapato yote ya mashamba yake katika muda huo wote wa miaka saba.

7. Baadaye Elisha alikwenda Damasko. Wakati huo mfalme Ben-hadadi alikuwa mgonjwa na alipoambiwa kwamba Elisha alikuwa Damasko,

8. alimwambia ofisa wake Hazaeli, “Mpelekee mtu wa Mungu zawadi umwambie atafute shauri kwa Mwenyezi-Mungu kama nitapona au la.”

9. Hazaeli akapakia zawadi za kila aina ya mazao ya Damasko kiasi cha mizigo ya ngamia arubaini na kumpelekea Elisha. Alipofika kwa Elisha alimwambia, “Mtumishi wako, Ben-hadadi, mfalme wa Aramu amenituma kwako; yeye anauliza, ‘Nitapona ugonjwa huu?’”

10. Basi Elisha akamjibu, “Atapona; lakini Mwenyezi-Mungu amenionesha kwamba atakufa.”

11. Ndipo Elisha akamkazia macho akiwa na hofu hata Hazaeli akashikwa na wasiwasi. Ghafla, Elisha mtu wa Mungu, akaanza kulia.

12. Hazaeli akamwuliza, “Bwana wangu, mbona unalia?” Elisha akamjibu, “Kwa sababu ninajua maovu ambayo utawatendea watu wa Israeli. Utateketeza ngome zao kwa moto, na kuwaua vijana wao, utawapondaponda watoto wao na kuwararua wanawake waja wazito.”

13. Hazaeli akauliza, “Lakini mimi mtumishi wako ni kitu kweli? Mimi niliye mbwa tu nitawezaje kutenda mambo hayo makubwa?” Elisha akamjibu, “Mwenyezi-Mungu amenionesha kwamba utakuwa mfalme wa Aramu.”

14. Ndipo Hazaeli alipotoka kwa Elisha, akarudi kwa bwana wake. Mfalme Ben-hadadi akamwuliza, “Elisha alikuambia nini?” Hazaeli akamjibu, “Aliniambia ya kwamba hakika utapona.”

15. Lakini kesho yake Hazaeli akachukua blanketi akalilowesha majini, kisha akamfunika nalo usoni mpaka akafa. Hazaeli akatawala Aramu mahali pake.

16. Mnamo mwaka wa tano wa utawala wa Yoramu mwana wa Ahabu, mfalme wa Israeli, Yehoramu mwana wa Yehoshafati, mfalme wa Yuda alianza kutawala.

17. Alianza kutawala akiwa na umri wa miaka thelathini na miwili. Alitawala huko Yerusalemu miaka minane.

Kusoma sura kamili 2 Wafalme 8