Agano la Kale

Agano Jipya

2 Wafalme 7:4-11 Biblia Habari Njema (BHN)

4. Hakuna maana ya kuingia mjini kwa sababu huko tutakufa. Kwa hiyo hebu twende kwenye kambi ya Waaramu; inawezekana wakatuua, au wasituue.”

5. Hivyo, giza lilipoanza kuingia, wakaenda kwenye kambi ya Waaramu, lakini walipofika huko, hapakuwa na mtu.

6. Maana Mwenyezi-Mungu alilifanya jeshi la Waaramu lisikie sauti kama ya jeshi kubwa lililokuwa na magari na farasi. Waaramu wakadhani kuwa mfalme wa Israeli amekodisha majeshi ya Wahiti na Wamisri kuja kuwashambulia.

7. Basi, katika usiku huo, Waaramu walikimbia wote ili kuyaokoa maisha yao wakiacha mahema yao, farasi na punda wao, na hata kambi yao jinsi ilivyokuwa.

8. Wakoma wale wanne walipofika pembeni mwa kambi, waliingia ndani ya hema moja, wakala na kunywa vile walivyopata humo, wakachukua fedha, dhahabu na nguo, wakaenda kuzificha. Wakaingia katika hema nyingine na kufanya vivyo hivyo.

9. Lakini wakaambiana, “Tunalofanya si sawa! Hii ni habari njema tuliyo nayo leo, na ikiwa tutangoja mpaka asubuhi, bila shaka tutaadhibiwa. Twende mara moja tukawaambie watu wa nyumba ya mfalme!”

10. Hivyo, wakaondoka katika kambi ya Waaramu na kuwaita mabawabu wa mji na kuwaambia: “Tulikwenda katika kambi ya Waaramu na hatukuweza kumwona wala kumsikia mtu yeyote. Farasi na punda wangali wamefungwa, na mahema yako kama walivyoyaacha.”

11. Walinda malango wakaeneza habari hizi mpaka zikafika nyumbani kwa mfalme.

Kusoma sura kamili 2 Wafalme 7