Agano la Kale

Agano Jipya

2 Wafalme 7:13-20 Biblia Habari Njema (BHN)

13. Mmoja kati ya maofisa wake akasema, “Watu wengi tayari wameangamia kama vile wale ambao wamekwisha fariki. Tafadhali utume watu wachache na farasi watano wa wale waliobaki ili waende kuona kumetokea nini.”

14. Wakachagua watu na kuwapa magari mawili. Mfalme akawatuma kuwafuata Waaramu, akisema, “Nendeni mkaone.”

15. Watu hao wakaenda mpaka Yordani na njiani waliona nguo na vifaa vingine Waaramu walivyoacha walipokuwa wanakimbia. Wakarudi na kumpasha mfalme habari.

16. Watu wa Samaria wakatoka na kuteka nyara kambi ya Waaramu. Kama vile Mwenyezi-Mungu alivyosema: Kilo tano za unga safi wa ngano au kilo kumi za shayiri ziliuzwa kwa kipande kimoja cha fedha.

17. Naye mfalme alikuwa amemweka ofisa mlinzi wake kulinda lango la mji. Ofisa huyo alikanyagwa papo hapo langoni na kuuawa na watu, kama vile Elisha mtu wa Mungu alivyotabiri wakati mfalme alipokwenda kumwona.

18. Elisha alikuwa amemwambia mfalme kwamba wakati kama huo siku iliyofuata, kilo tano za unga mzuri wa ngano au kilo kumi za shayiri zingeuzwa kwa kipande kimoja cha fedha; lakini hapo awali

19. kapteni alikuwa amembishia Elisha, akisema, “Kama Mwenyezi-Mungu mwenyewe angefanya madirisha mbinguni, je, jambo hili lingewezekana?” Naye Elisha alikuwa amemjibu, “Utaona yakitendeka, lakini chakula chenyewe hutakila.”

20. Na hivyo ndivyo ilivyotokea – kapteni akafa kwa kukanyagwa na watu kwenye lango la mji.

Kusoma sura kamili 2 Wafalme 7