Agano la Kale

Agano Jipya

2 Wafalme 18:16-31 Biblia Habari Njema (BHN)

16. kadhalika, alingoa dhahabu kutoka katika milango ya hekalu la Mwenyezi-Mungu na ile dhahabu ambayo yeye mwenyewe aliiweka kwenye mihimili ya mlango; yote akampelekea Senakeribu.

17. Kisha mfalme wa Ashuru alimtuma jemadari mkuu, amiri mkuu, mkuu wa matowashi pamoja na jeshi kubwa kutoka Lakishi kwenda kwa mfalme Hezekia huko Yerusalemu. Walisafiri na kufika Yerusalemu. Nao walipowasili waliingia na kusimama karibu na mfereji wa bwawa lililoko upande wa juu katika barabara kuu inayoelekea Uwanda wa Dobi.

18. Walipomwita mfalme Hezekia walilakiwa na Eliakimu mwana wa Hilkia, ambaye alikuwa msimamizi wa ikulu; Shebna, aliyekuwa katibu na Yoa mwana wa Asafu, mwandishi wa kumbukumbu za mfalme.

19. Ndipo jemadari mkuu alipowaambia, “Mwambieni Hezekia, hivi ndivyo anavyosema mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru: Ni ujasiri wa namna gani huu unaouwekea matumaini?

20. Je, unadhani kuwa maneno matupu ndiyo maarifa na nguvu katika vita? Ni nani unayemtegemea hata ukaniasi?

21. Angalia, sasa, unategemea Misri, utete uliovunjika ambao utamchoma mkono yeyote atakayeutegemea. Hivyo ndivyo Farao mfalme wa Misri alivyo kwa wote wale wanaomtegemea.”

22. “Lakini hata kama mkiniambia: ‘Tunamtegemea Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu’, Jueni kwamba ni Mungu huyohuyo ambaye Hezekia alipaharibu mahali pake pa juu na madhabahu zake, akawaambia watu wa Yuda na watu wa Yerusalemu waabudu tu mbele ya madhabahu iliyoko Yerusalemu.

23. Basi, fanyeni mkataba na bwana wangu mfalme wa Ashuru, nami nitawapa farasi 2,000 kama mtaweza kupata wapandafarasi.

24. Mwawezaje kumrudisha nyuma ofisa mmoja kati ya watumishi wa bwana wangu walio na cheo cha chini kabisa, wakati mnategemea Misri iwaletee magari na wapandafarasi?”

25. Zaidi ya hayo, je, mnafikiri nimekuja bila amri ya Mwenyezi-Mungu ili kuishambulia na kuiangamiza nchi hii? Mwenyezi-Mungu ndiye aliyeniambia, “Ishambulie nchi hii na kuiangamiza!”

26. Basi, Eliakimu mwana wa Hilkia, Shebna na Yoa wakamwambia huyo jemadari mkuu, “Tafadhali, sema nasi kwa lugha ya Kiaramu, maana tunaielewa; usiseme nasi kwa lugha ya Kiebrania; kwa kuwa watu walioko ukutani wanasikiliza.”

27. Yule jemadari mkuu akawaambia, “Je, bwana wangu amenituma kutoa ujumbe huu kwa bwana wenu na kwenu tu? Je, hakunituma pia kwa watu wanaokaa ukutani ambao wamehukumiwa pamoja nanyi kula mavi yao wenyewe na kunywa mikojo yao wenyewe?”

28. Kisha huyo mkuu wa matowashi akasimama, akapaza sauti na kusema kwa lugha ya Kiebrania, “Sikilizeni maneno ya mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru!

29. Hivi ndivyo anavyosema mfalme: Msikubali Hezekia awadanganye, kwa sababu hataweza kuwaokoa mikononi mwa mfalme.

30. Msikubali awashawishi ili mumtegemee Mwenyezi-Mungu akisema, ‘Mwenyezi-Mungu atatuokoa na mji huu hautatiwa mikononi mwa mfalme wa Ashuru.’

31. Msimsikilize Hezekia, maana mfalme wa Ashuru anasema, ‘Muwe na amani nami, na jisalimisheni kwangu. Hapo kila mmoja wenu ataweza kula matunda ya mzabibu wake mwenyewe, matunda ya mtini wake mwenyewe, na kunywa maji ya kisima chake mwenyewe,

Kusoma sura kamili 2 Wafalme 18