Agano la Kale

Agano Jipya

2 Wafalme 17:15-24 Biblia Habari Njema (BHN)

15. Walikataa kutii maagizo yake; hawakushika agano alilofanya na babu zao; licha ya kupuuza maonyo yake, waliabudu sanamu zisizokuwa na maana mpaka hata wao wenyewe hawakuwa na maana tena; walifuata desturi za mataifa yaliyowazunguka: Walipuuza amri za Mwenyezi-Mungu; wala hawakuzizingatia.

16. Walivunja amri zote za Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, wakatengeneza sanamu za miungu ya ndama wawili wa kusubu; vilevile wakatengeneza sanamu za mungu wa kike Ashera wakaabudu na vitu vyote vya angani na wakamtumikia Baali.

17. Waliwatambika watoto wao wa kiume na wa kike kwa miungu ya uongo; wakataka shauri kwa watabiri na wachawi. Walinuia kabisa kutenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, wakamkasirisha sana.

18. Basi, Mwenyezi-Mungu akawakasirikia sana watu wa Israeli na kuwafukuza kabisa mbele yake; hakuacha mtu isipokuwa kabila la Yuda peke yake.

19. Lakini hata watu wa Yuda hawakutii amri za Mwenyezi-Mungu, Mungu wao; bali walifuata desturi zilizoletwa na watu wa Israeli.

20. Mwenyezi-Mungu aliwakataa Waisraeli wote; akawaadhibu na kuwaacha mikononi mwa adui wakali, na kisha akawafukuza mbele yake.

21. Baada ya Mwenyezi-Mungu kutenga watu wa Israeli kutoka ukoo wa Daudi, walimtawaza Yeroboamu mwana wa Nebati kuwa mfalme. Naye Yeroboamu aliwafanya watu wa Israeli kumwacha Mwenyezi-Mungu na kutenda dhambi kubwa sana.

22. Waisraeli walitenda dhambi alizotenda Yeroboamu; hawakuweza kuziacha,

23. hadi hatimaye Mwenyezi-Mungu akawafukuza kutoka mbele yake, kama vile alivyokuwa amesema kupitia kwa watumishi wake wote manabii. Kwa hiyo watu wa Israeli walichukuliwa mateka kutoka nchi yao wenyewe mpaka Ashuru ambako wanakaa hata sasa.

24. Kisha mfalme wa Ashuru akachukua watu kutoka Babuloni, Kutha, Ava, Hamathi na Sefarvaimu na kuwaweka katika miji ya Samaria mahali pa watu wa Israeli waliopelekwa uhamishoni. Wakaitwaa miji hiyo na kukaa humo.

Kusoma sura kamili 2 Wafalme 17