Agano la Kale

Agano Jipya

2 Wafalme 12:1-16 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Katika mwaka wa saba wa enzi ya mfalme Yehu wa Israeli Yoashi alianza kutawala Yuda huko Yerusalemu, naye akatawala kwa muda wa miaka arubaini huko Yerusalemu. Mama yake alikuwa Sibia, kutoka Beer-sheba.

2. Wakati wa maisha yake yote alitenda mema mbele ya Mwenyezi-Mungu, kwa sababu kuhani Yehoyada alikuwa akimfundisha.

3. Hata hivyo, mahali pa juu pa kuabudia miungu hapakuharibiwa, na watu waliendelea kutambika na kufukiza ubani huko.

4. Yoashi akaita makuhani na kuwaamuru, akisema, “Fedha yote inayoletwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu ikiwa imetokana na uuzaji wa vitu vitakatifu, fedha ya kila mtu kadiri alivyoandikiwa, na fedha ambayo mtu huvutwa kuitoa kwa hiari katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu,

5. makuhani wazipokee kutoka kwa kila mtu; nao warekebishe nyumba popote panapohitajika marekebisho.”

6. Lakini hata baada ya miaka ishirini na mitatu ya mfalme Yoashi makuhani walikuwa bado hawajafanya marekebisho yoyote ya nyumba.

7. Kwa hiyo mfalme Yoashi alimwita kuhani Yehoyada na makuhani wengine na kuwauliza, “Mbona hamrekebishi nyumba? Basi, msichukue fedha kutoka kwa watu mnaowatumikia, bali mtazileta, ili nyumba irekebishwe.”

8. Makuhani wakakubali wasipokee fedha tena kutoka kwa watu na pia wakaahidi kutofanya marekebisho ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu.

9. Yehoyada akachukua sanduku na kutoboa tundu kwenye kifuniko chake, kisha akaliweka kwenye madhabahu upande wa kulia, mtu anapoingia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Nao makuhani waliokuwa katika zamu langoni waliweka fedha zote zilizoletwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu.

10. Kila walipoona kuwa mna fedha nyingi sandukuni, katibu wa mfalme na kuhani mkuu waliingia na kuhesabu na kuzifunga katika vifurushi fedha zote zilizopatikana katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu.

11. Kisha baada ya kuzipima waliwapa wafanyakazi waliosimamia nyumba ya Mwenyezi-Mungu, nao wakawalipa maseremala na wajenzi, waliorekebisha nyumba ya Mwenyezi-Mungu;

12. pia waashi na wakata-mawe, zikatumiwa kununulia mbao na mawe yaliyochongwa ili kufanyia marekebisho nyumba ya Mwenyezi-Mungu na kutimiza mahitaji mengine yote ya marekebisho ya nyumba.

13. Lakini pesa hizo hazikutumiwa kwa kulipia utengenezaji wa mabirika ya fedha, mikasi ya kukatia tambi za mishumaa, mabakuli, tarumbeta, wala kwa vyombo vingine vyovyote vya dhahabu au vya fedha.

14. Zote zilitumiwa kwa kuwalipa wafanyakazi waliozitumia kufanya marekebisho ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu.

15. Wafanyakazi waliosimamia kazi hii walikuwa waaminifu kabisa, kwa hiyo hapakuwa na haja ya kuwataka watoe hesabu ya matumizi ya fedha hizo.

16. Fedha zilizotolewa kuwa sadaka za hatia na sadaka za kuondoa dhambi hazikuingizwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu; hizo zilikuwa ni mali ya makuhani.

Kusoma sura kamili 2 Wafalme 12