Agano la Kale

Agano Jipya

2 Samueli 20:3-15 Biblia Habari Njema (BHN)

3. Hatimaye, Daudi aliwasili nyumbani kwake mjini Yerusalemu. Mfalme aliwachukua masuria wake kumi ambao alikuwa amewaacha kuangalia nyumba yake, akawaweka kwenye nyumba moja chini ya ulinzi, akawatunza vizuri, lakini hakulala nao. Hivyo, masuria hao wakawa wametiwa ndani hadi siku za kufa kwao, wakaishi kana kwamba, walikuwa wajane.

4. Kisha, mfalme akamwambia Amasa, “Nikusanyie watu wote wa Yuda katika siku tatu, na wewe mwenyewe uwepo.”

5. Basi, Amasa akaenda kuwaita watu wa Yuda. Lakini akachelewa kurudi katika wakati ule aliopangiwa na mfalme.

6. Daudi akamwambia Abishai, “Sasa, Sheba mwana wa Bikri, atatuletea madhara kuliko Absalomu. Chukua watumishi wangu, umfuatie Sheba asije akaingia kwenye miji yenye ngome akaponyoka, tusimwone tena.”

7. Abishai akatoka akiwa pamoja na Yoabu, Wakerethi na Wapelethi pamoja na mashujaa wote. Hao wote waliondoka Yerusalemu kwenda kumfuatia Sheba mwana wa Bikri.

8. Walipofika kwenye jiwe kubwa lililoko huko Gibeoni, Amasa akatoka kuwalaki. Yoabu alikuwa amevaa vazi la kijeshi, na ndani ya vazi hilo kulikuwa na mkanda ulioshikilia upanga kiunoni mwake ukiwa kwenye ala yake. Yoabu alipokuwa anakaribia, upanga wake ulichomoka alani ukaanguka chini.

9. Yoabu akamwambia Amasa, “Je, hujambo ndugu yangu?” Yoabu akamshika Amasa kidevuni kwa mkono wa kulia kana kwamba anataka kumbusu.

10. Lakini Amasa hakuona upanga uliokuwa mkononi mwa Yoabu. Basi, Yoabu akamchoma Amasa upanga tumboni, matumbo yake yakatoka nje, akafa. Yoabu hakumchoma upanga mara mbili.Kisha, Yoabu na nduguye Abishai wakaendelea kumfuatilia Sheba mwana wa Bikri.

11. Mtu mmoja wa Yoabu akaja akasimama karibu na mwili wa Amasa, akasema, “Yeyote anayempenda Yoabu na yeyote anayempenda Daudi, na amfuate Yoabu!”

12. Amasa alikuwa bado anagagaa kwenye damu yake katikati ya barabara kuu. Kwa hiyo, kila mtu aliyepita hapo, alipomwona, alisimama. Lakini yule mtu alipoona kwamba watu wote walikuja na kusimama hapo, aliuondoa mwili wa Amasa barabarani, akaupeleka shambani na kuufunika kwa nguo.

13. Amasa alipoondolewa kwenye barabara kuu, watu wote sasa waliendelea kumfuata Yoabu kumfuatia Sheba mwana wa Bikri.

14. Sheba alipitia katika makabila yote ya Israeli mpaka mji wa Abeli wa Beth-maaka. Watu wote wa ukoo wa Bikri wakakusanyika na kumfuata.

15. Watu wote waliokuwa pamoja na Yoabu wakaenda kumzingira Sheba akiwa katika mji huo wa Abeli wa Beth-maaka. Walirundika kuuzingira mji, na ngome; halafu wakaanza kuubomoa ukuta ili kuuangusha chini.

Kusoma sura kamili 2 Samueli 20