Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wafalme 9:11-27 Biblia Habari Njema (BHN)

11. mfalme Solomoni alimpa Hiramu mfalme wa Tiro, miji ishirini katika mkoa wa Galilaya (kwa sababu huyo Hiramu alikuwa amempelekea Solomoni mbao za mierezi na miberoshi, na dhahabu pia, kadiri alivyohitaji kwa ujenzi).

12. Lakini Hiramu alipowasili kutoka Tiro na kuiona miji hiyo aliyokuwa amepewa na Solomoni hakupendezwa nayo.

13. Basi, akamwuliza Solomoni, “Ndugu yangu, ni miji gani hii ambayo umenipa?” Ndio sababu miji hiyo inaitwa nchi ya Kabuli hata leo.

14. Hiramu alikuwa amempelekea mfalme Solomoni dhahabu kilo 3,600.

15. Yafuatayo ni maelezo juu ya jinsi mfalme Solomoni alivyotumia kazi za kulazimishwa kujenga nyumba ya Mwenyezi-Mungu, ikulu yake, ngome ya Milo na ukuta wa Yerusalemu, na pia katika kujenga upya miji ya Hazori, Megido na Gezeri;

16. (Gezeri ndio mji ambao Farao, mfalme wa Misri, alikuwa ameuteka, akauchoma moto na kuwaua Wakanaani, wakazi wake. Baadaye, binti Farao alipoolewa na Solomoni, mfalme wa Misri alimpa binti yake mji huo wa Gezeri uwe zawadi ya harusi.

17. Basi, Solomoni aliujenga upya mji wa Gezeri); hali kadhalika alijenga Beth-horoni ya chini;

18. kadhalika miji ifuatayo: Baalathi, na Tamari, mji ulio nyikani katika nchi ya Yuda

19. na miji yake yote ya ghala, magari yake ya kukokotwa, na wapandafarasi wake; pia chochote alichotaka kujenga katika Yerusalemu, Lebanoni au kwingineko katika ufalme wake.

20. Watu wengine wote waliobaki miongoni mwa Waamori, Wahiti, Waperizi, Wahivi na Wayebusi, yaani wote hao ambao hawakuwa wa taifa la Israeli,

21. pamoja na wazawa wao ambao Waisraeli hawakuweza kuwaangamiza kabisa, Solomoni aliwafanyiza kazi za kulazimishwa hata leo.

22. Lakini kati ya Waisraeli, Solomoni hakumfanya mtu yeyote kuwa mtumwa; wao ndio waliokuwa askari, watumishi wake, makamanda wake, maofisa wake, makamanda wa magari yake ya kukokotwa, na wapandafarasi wake.

23. Ifuatayo ndiyo jumla ya maofisa wakuu waliohusika na uangalizi wa kazi ya Solomoni: Watu 550, hao ndio waliosimamia watu waliofanya kazi.

24. Baadaye binti Farao aliuhama mji wa Daudi, akaenda kukaa katika nyumba yake mwenyewe ambayo Solomoni alimjengea; kisha Solomoni akajenga ngome ya Milo.

25. Mara tatu kila mwaka, Solomoni alitoa tambiko za kuteketezwa na tambiko za amani juu ya madhabahu aliyokuwa amemjengea Mwenyezi-Mungu, akamfukizia Mwenyezi-Mungu ubani; pia alifanya marekebisho ya nyumba.

26. Mfalme Solomoni aliunda merikebu nyingi huko Esion-geberi, karibu na Elothi iliyo pwani ya Bahari ya Shamu, katika nchi ya Edomu.

27. Naye mfalme Hiramu akawatuma maofisa wake na mabaharia pamoja na watumishi wa Solomoni.

Kusoma sura kamili 1 Wafalme 9