Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wafalme 14:3-19 Biblia Habari Njema (BHN)

3. Mpelekee mikate kumi, maandazi kadha, na asali chupa moja. Yeye atakuambia yatakayompata mtoto wetu.”

4. Basi, mkewe Yeroboamu akaondoka, akaenda Shilo nyumbani kwa Ahiya. Wakati huo, Ahiya alikuwa hawezi tena kuona sawasawa kwa sababu ya uzee.

5. Mwenyezi-Mungu alikuwa amekwisha mwambia Ahiya kwamba mke wa Yeroboamu alikuwa njiani, anakuja kumwuliza yatakayompata mwanawe mgonjwa, na jinsi atakavyomjibu.Mkewe Yeroboamu alipofika, alijisingizia kuwa mtu mwingine.

6. Lakini Ahiya alipomsikia anaingia mlangoni, alisema, “Karibu ndani mke wa Yeroboamu. Lakini mbona unajisingizia kuwa mtu mwingine? Ninao ujumbe usio mzuri kwako!

7. Nenda ukamwambie Yeroboamu kwamba Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, asema hivi: ‘Nilikuteua miongoni mwa watu, nikakufanya kuwa kiongozi wa watu wangu, Israeli;

8. nikaurarua ufalme utoke kwa wazawa wa Daudi, nikakupa wewe. Lakini wewe ni kinyume kabisa cha mtumishi wangu Daudi ambaye alizishika amri zangu, akafuata matakwa yangu kwa moyo wake wote na kutenda tu yaliyo sawa mbele ya macho yangu.

9. Wewe umetenda uovu mbaya zaidi kuliko waliotenda wale waliokutangulia; wewe umenikasirisha kwa kujitengenezea miungu mingine na sanamu za kufua, kisha umeniacha.

10. Haya basi, sasa nitailetea balaa jamaa hii yake, Yeroboamu, nitawaua wanaume wote wa jamaa zake katika Israeli, awe mtumwa au huru. Jamaa wake wote nitawateketeza kama mtu ateketezavyo mavi, mpaka yatoweke.

11. Yeyote aliye wa jamaa ya Yeroboamu atakayefia mjini, mbwa watamla; na yeyote atakayefia shambani, ndege wa angani watamla. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.’”

12. Ahiya akamwambia mkewe Yeroboamu, “Haya inuka, uende zako nyumbani. Mara tu utakapoingia mjini, mwanao atakufa.

13. Watu wote wa Israeli watafanya matanga na kumzika. Walakini, ni huyo tu wa jamaa ya Yeroboamu atakayezikwa, kwani ni yeye tu wa jamaa ya Yeroboamu aliyepata kumpendeza Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli.

14. Tena leo hii, Mwenyezi-Mungu ataweka mfalme mwingine katika Israeli ambaye ataikatilia mbali jamaa ya Yeroboamu.

15. Naam, tangu sasa, Mwenyezi-Mungu atawapiga watu wa Israeli, nao watatikisika kama unyasi unavyotikiswa mtoni. Atawangoa kutoka nchi hii nzuri aliyowapa babu zao, na kuwatawanya mbali, ngambo ya mto Eufrate, kwa sababu wamemkasirisha Mwenyezi-Mungu kwa kujitengenezea sanamu za Ashera, mungu wa kike.

16. Mwenyezi-Mungu ataitupa Israeli kwa sababu ya dhambi alizotenda Yeroboamu, na kuwafanya watu wa Israeli pia watende dhambi.”

17. Hapo, mkewe Yeroboamu akaondoka, akashika safari mpaka Tirza. Mara tu alipofika mlangoni, mtoto akafa.

18. Watu wote wa Israeli wakamzika na kufanya matanga kama alivyosema Mwenyezi-Mungu, kwa njia ya nabii Ahiya, mtumishi wake.

19. Matendo mengine ya mfalme Yeroboamu, jinsi alivyopigana vita na alivyotawala, yote yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Israeli.

Kusoma sura kamili 1 Wafalme 14