Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wafalme 13:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Siku moja Yeroboamu alikuwa amesimama kando ya madhabahu ili afukize ubani. Basi, mtu wa Mungu kutoka Yuda akawasili hapo Betheli na ujumbe wa Mwenyezi-Mungu.

2. Mtu huyo akailaani ile madhabahu akisema, “Ee madhabahu! Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Atazaliwa mtoto katika ukoo wa Daudi, jina lake Yosia. Huyo atawatwaa makuhani wanaohudumu mahali pa ibada na kufukiza ubani juu yako, na kutambika juu yako; naam, mifupa ya watu itateketezwa juu yako!’”

3. Mtu huyo akatoa ishara siku ileile, akasema: “Hii ndiyo ishara aliyotamka Mwenyezi-Mungu: ‘Madhabahu itabomoka, na majivu yaliyo juu yake yatamwagika.’”

4. Mfalme Yeroboamu aliposikia maneno hayo ya mtu wa Mungu dhidi ya madhabahu huko Betheli, alinyosha mkono akasema, “Mkamateni huyo!” Na mara huo mkono wake aliounyosha, ukakauka, asiweze tena kuukunja.

5. Madhabahu nayo ikabomoka, na majivu yake yakamwagika chini, kama ishara ile aliyoitoa huyo mtu wa Mungu na ujumbe wa Mwenyezi-Mungu.

6. Basi, mfalme Yeroboamu akamwambia nabii, “Tafadhali, umsihi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, uniombee mkono wangu upate kupona.” Naye nabii akamwomba Mwenyezi-Mungu, na mkono wa mfalme ukapona, ukarudia hali yake ya hapo awali.

7. Ndipo mfalme akamwambia mtu wa Mungu, “Karibu nyumbani kwangu kula chakula, nami nikupe zawadi.”

8. Lakini mtu wa Mungu akamwambia, “Hata kama ukinipa nusu ya milki yako, sitakwenda pamoja nawe. Sitakula wala kunywa maji mahali hapa,

9. kwani Mwenyezi-Mungu aliniamuru nisile chakula au kunywa maji, wala nisirudi kwa njia ileile niliyoifuata kuja hapa.”

10. Basi, mtu huyo akaenda zake, wala hakurudi kwa njia ile aliyoijia Betheli.

11. Wakati huo, palikuwa na nabii mmoja mzee huko Betheli. Wanawe wakamwendea, wakamweleza mambo yote aliyotenda yule mtu wa Mungu siku hiyo, huko Betheli; wakamwambia pia yale maneno yule mtu aliyomwambia mfalme Yeroboamu.

12. Baba yao akawauliza, “Amefuata njia ipi?” Nao wakamwonesha njia aliyoifuata huyo mtu wa Mungu kutoka Yuda.

13. Naye akawaambia watoto wake, “Nitandikieni huyo punda.” Nao wakamtandikia punda, na mzee akapanda juu yake.

Kusoma sura kamili 1 Wafalme 13