Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wafalme 11:12-27 Biblia Habari Njema (BHN)

12. Hata hivyo, kwa ajili ya baba yako Daudi, sitafanya hivyo maishani mwako, bali nitauondoa utawala huo mikononi mwa mwanao.

13. Hata yeye sitamnyanganya milki yote, bali nitamwachia mwanao kabila moja, kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi, na kwa ajili ya mji wa Yerusalemu ambao nimeuchagua kuwa wangu.”

14. Ndipo Mwenyezi-Mungu akamfanya Hadadi aliyekuwa wa ukoo wa mfalme wa Edomu, kuwa adui ya Solomoni.

15. Wakati Daudi alipowaangamiza Waedomu Yoabu, mkuu wa jeshi la Daudi, alikwenda huko kuwazika waliouawa. Yoabu aliwaua wanaume wote wa Edomu.

16. (Yoabu alikaa huko na wanajeshi wake kwa muda wa miezi sita, apate kuwaangamiza kabisa wanaume wote wa Edomu.)

17. Lakini Hadadi ambaye wakati huo alikuwa kijana alitorokea Misri pamoja na Waedomu kadhaa, watumishi wa baba yake.

18. Hadadi na wenzake walisafiri kutoka Midiani, wakawachukua watu wengine huko Parani, wakaenda nao mpaka Misri, kwa Farao mfalme wa nchi hiyo. Farao akampatia Hadadi nyumba, akaamuru awe akipewa chakula, akampa na ardhi.

19. Farao alipendezwa sana na Hadadi. Hivyo Farao akamruhusu shemeji yake, mdogo wa malkia Tapenesi, aolewe na Hadadi.

20. Huyo dada wa Tapenesi akamzalia Hadadi mwana aliyeitwa Genubathi. Genubathi alilelewa na Tapenesi katika nyumba ya Farao, pamoja na wana wa mfalme.

21. Lakini Hadadi aliposikia huko Misri kwamba Daudi na Yoabu mkuu wa jeshi, walikuwa wamefariki, alimwambia Farao, “Uniruhusu niondoke nirudi nchini kwangu.”

22. Lakini Farao akamwuliza, “Nimekunyima nini hata uamue sasa kurudi nchini kwako?” Naye Hadadi akamsihi akisema, “Uniache tu niende.”

23. Vilevile, Mungu alimfanya Rezoni mwana wa Eliada, awe adui ya Solomoni. Rezoni alikuwa amemtoroka bwana wake, mfalme Hadadezeri wa Soba.

24. Baada ya Daudi kufanya mauaji huko Soba, Rezoni alikusanya watu na kuunda genge la maharamia, naye mwenyewe akawa kiongozi wao. Basi, wakaenda Damasko, wakakaa huko na kumfanya Rezoni mfalme wa Damasko.

25. Rezoni alikuwa adui wa Israeli siku zote za utawala wa Solomoni, akamsumbua sana Solomoni kama naye Hadadi alivyomsumbua. Basi, Rezoni aliidharau Israeli, naye alitawala nchi ya Aramu.

26. Yeroboamu mwana wa Nebati, Mwefraimu wa Sereda, mtumishi wa Solomoni, ambaye mama yake mjane, aliitwa Zerua, pia alimwasi mfalme.

27. Kisa cha uasi huo ni hiki: Solomoni alipokuwa akishughulika na kusawazisha sehemu ya Milo, na kuimarisha kuta za mji wa baba yake Daudi,

Kusoma sura kamili 1 Wafalme 11