Agano la Kale

Agano Jipya

1 Samueli 14:34-48 Biblia Habari Njema (BHN)

34. Akawaambia, “Nendeni mkawaambie watu wote walete ng'ombe na kondoo wao hapa, wawachinje na kuwala hapa. Wasitende dhambi dhidi ya Mwenyezi-Mungu, kwa kula nyama yenye damu.” Hivyo, usiku ule wote walipeleka ng'ombe wao na kuwachinjia hapo.

35. Basi, Shauli akamjengea Mwenyezi-Mungu madhabahu. Hiyo ilikuwa ndiyo madhabahu ya kwanza ambayo Shauli alimjengea Mwenyezi-Mungu.

36. Kisha Shauli akawaambia watu, “Twendeni tukawafuatie Wafilisti usiku, tukawavamie na kupora mali zao mpaka asubuhi; hatutamwacha mtu yeyote hai.” Watu wakamwambia, “Fanya unachoona kuwa chema kwako.” Lakini kuhani akawaambia, “Kwanza tuombe shauri kwa Mwenyezi-Mungu.”

37. Hivyo, Shauli akamwuliza Mungu, “Je, niende kuwashambulia Wafilisti? Je, utawatia mikononi mwa Waisraeli?” Lakini Mungu hakujibu kitu siku hiyo.

38. Shauli akasema, “Njoni hapa enyi viongozi wa watu, tujue ni dhambi gani tumetenda leo.

39. Naapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai na ambaye huiokoa Israeli, hata kama ni mwanangu Yonathani, lazima auawe.” Lakini hakuna mtu aliyesema neno.

40. Hivyo, Shauli akawaambia, “Nyinyi nyote simameni upande ule, halafu mimi na Yonathani mwanangu tutasimama upande huu.” Wao wakajibu, “Fanya chochote unachoona kinafaa.”

41. Shauli akasema, “Ee Mwenyezi-Mungu wa Israeli, kwa nini hujanijibu mimi mtumishi wako? Ee Mwenyezi-Mungu wa Israeli, ikiwa hatia iko kwangu au kwa Yonathani mwanangu, basi, amua kwa jiwe la kauli ya Urimu. Lakini ikiwa hatia hiyo iko kwa watu wako wa Israeli, amua kwa jiwe la kauli ya Thumimu.” Yonathani na Shauli walipatikana kuwa na hatia, lakini watu walionekana hawana hatia.

42. Shauli akasema, “Pigeni kura kati yangu na mwanangu Yonathani.” Yonathani akapatikana kuwa na hatia.

43. Ndipo Shauli akamwambia Yonathani, “Niambie ulilofanya.” Yonathani akajibu, “Nilikula asali kidogo kwa kutumia fimbo yangu. Niko hapa na niko tayari kufa.”

44. Shauli akasema, “Mungu na anitendee mimi vivyo hivyo na hata na wengine. Yonathani ni lazima utauawa.”

45. Lakini watu wakamwambia Shauli, “Mbona Yonathani aliyeiletea Israeli ushindi huu mkubwa, auawe? Jambo hilo liwe mbali. Twaapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, hata unywele wa kichwa chake hautaanguka chini. Alichokifanya leo, amekifanya kwa msaada wa Mwenyezi-Mungu.” Hivyo, watu walimkomboa Yonathani naye hakuuawa.

46. Kisha Shauli aliacha kuwafuatia Wafilisti, nao Wafilisti wakarudi makwao.

47. Baada ya Shauli kuwa mfalme wa Israeli, alipigana na adui zake kila upande: Wamoabu, Waamoni, Waedomu, wafalme wa Soba, na Wafilisti. Kila alipopigana vita, alishinda.

48. Alipigana kwa uhodari, akawashinda Waamaleki. Aliwaokoa Waisraeli kutoka kwa watu wote waliowashambulia.

Kusoma sura kamili 1 Samueli 14