Agano la Kale

Agano Jipya

Waroma 4:2-17 Biblia Habari Njema (BHN)

2. Kama Abrahamu alikuwa amefanywa mwadilifu kutokana na bidii yake, basi, anacho kitu cha kujivunia mbele ya Mungu.

3. Kwa maana, Maandiko Matakatifu yasema: “Abrahamu alimwamini Mungu, naye Mungu akamkubali kuwa mwadilifu.”

4. Mfanyakazi hulipwa mshahara; mshahara wake si zawadi bali ni haki yake.

5. Lakini mtu asiyetegemea matendo yake mwenyewe, bali anamwamini Mungu ambaye huwasamehe waovu, basi, Mungu huijali imani ya mtu huyo, akamkubali kuwa mwadilifu.

6. Naye Daudi asema hivi juu ya furaha ya mtu yule ambaye Mungu amemkubali kuwa mwadilifu bila kuyajali matendo yake:

7. “Heri wale waliosamehewa makosa yaoambao makosa yao yamefutwa.

8. Heri mtu yule ambayeBwana hataziweka dhambi zake katika kumbukumbu.”

9. Je, hiyo ni kwa wale waliotahiriwa tu, ama pia kwa wale wasiotahiriwa? Ni kwa wale wasiotahiriwa pia. Kwa maana tumekwisha sema: “Abrahamu aliamini, naye Mungu akamkubali kuwa mwadilifu.”

10. Je, Abrahamu alikubaliwa kabla ya kutahiriwa, ama baada ya kutahiriwa? Kabla ya kutahiriwa, na si baada ya kutahiriwa.

11. Abrahamu alitahiriwa baadaye, na kutahiriwa huko kulikuwa alama iliyothibitisha kwamba Mungu alimkubali kuwa mwadilifu kwa sababu ya imani yake aliyokuwa nayo kabla ya kutahiriwa. Kwa hiyo, Abrahamu amekuwa baba wa wale wote ambao, ingawa hawakutahiriwa, wamemwamini Mungu, wakafanywa waadilifu.

12. Vilevile yeye ni baba wa wale waliotahiriwa; lakini si kwa kuwa wametahiriwa, bali kwa sababu wanafuata njia ileile ya imani baba yetu Abrahamu aliyofuata kabla ya kutahiriwa.

13. Mungu alimwahidi Abrahamu na wazawa wake kwamba ulimwengu ungekuwa mali yao. Ahadi hiyo haikufanywa kwa sababu Abrahamu aliitii sheria, bali kwa kuwa aliamini, akakubaliwa kuwa mwadilifu.

14. Maana kama watakaopewa hayo aliyoahidi Mungu ni wale tu wanaoitii sheria, basi, imani haina maana yoyote, nayo ahadi ya Mungu si kitu.

15. Sheria husababisha ghadhabu; lakini kama hakuna sheria, haiwezekani kuivunja.

16. Kwa sababu hiyo, jambo hili lategemea imani, hivyo kwamba ahadi hiyo yatokana na neema ya Mungu, na kwamba ni hakika kuwa ahadi hiyo ni kwa ajili ya wote: Si kwa wale tu wanaoishika sheria, bali pia kwa wale waishio kwa imani kama Abrahamu. Yeye ni baba yetu sisi sote.

17. Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Nimekuweka uwe baba wa mataifa mengi.” Ahadi hiyo ni kweli mbele ya Mungu ambaye Abrahamu alimwamini-Mungu ambaye huwapa wafu uhai, na kwa amri yake, vitu ambavyo havikuwapo huwa.

Kusoma sura kamili Waroma 4