Agano la Kale

Agano Jipya

2 Sam. 16:1-13 Swahili Union Version (SUV)

1. Naye Daudi alipokipita punde hicho kilele cha mlima, tazama, Siba, mtumwa wa Mefiboshethi, akamkuta, na punda wawili waliotandikwa, na juu yao mikate mia mbili ya ngano, na vishada mia vya zabibu kavu, na matunda mia ya wakati wa hari, na kiriba cha divai.

2. Mfalme akamwambia Siba, Ni za nini hizi? Siba akasema, Punda ni za jamaa ya mfalme wazipande; na mkate na matunda ni chakula cha hawa vijana; na divai ni kwamba wanywe hao wazimiao nyikani.

3. Mfalme akasema, Na mwana wa bwana wako yuko wapi? Siba akamwambia mfalme, Angalia, anakaa Yerusalemu; kwani alisema, Leo nyumba ya Israeli watanirudishia ufalme wa baba yangu.

4. Ndipo mfalme akamwambia Siba, Tazama, yote yaliyokuwa ni mali ya Mefiboshethi ni yako. Siba akasema, Mimi nasujudu; na nione kibali machoni pako, Ee bwana wangu, mfalme.

5. Basi mfalme Daudi alipofika Bahurimu, tazama, kulitoka huko mtu wa jamaa ya nyumba ya Sauli, jina lake akiitwa Shimei, mwana wa Gera; alitoka, akalaani alipokuwa akienda.

6. Tena akamtupia Daudi mawe, na watumishi wote wa mfalme Daudi; na watu wote na mashujaa wote walikuwako mkono wake wa kuume na mkono wake wa kushoto.

7. Na Shimei alipolaani, alisema hivi, Nenda zako! Nenda zako! Ewe mtu wa damu! Ewe mtu usiyefaa!

8. BWANA amerudisha juu yako damu yote ya nyumba ya Sauli ambaye umetawala badala yake; naye BWANA ametia ufalme katika mkono wa Absalomu mwanao; kisha, angalia, wewe umetwaliwa katika uovu wako mwenyewe, kwa sababu umekuwa mtu wa damu.

9. Ndipo Abishai mwana wa Seruya, akamwambia mfalme, Mbona mbwa mfu huyu amlaani mfalme bwana wangu? Na nivuke, nakusihi, nikaondoe kichwa chake.

10. Mfalme akasema, Nina nini na ninyi, enyi wana wa Seruya? Kwa sababu yeye analaani, na kwa sababu BWANA amemwambia, Mlaani Daudi, basi, ni nani atakayesema, Mbona umetenda haya?

11. Daudi akamwambia Abishai, na watumishi wake wote, Angalieni, huyu mwanangu, aliyetoka viunoni mwangu, anautafuta uhai wangu; si zaidi Mbenyamini huyu sasa? Mwacheni alaani, kwa sababu BWANA ndiye aliyemwagiza.

12. Labda BWANA atayaangalia mabaya yaliyonipata, naye BWANA atanilipa mema kwa sababu ya kunilaani kwake leo.

13. Basi wakaendelea njiani Daudi na watu wake; Shimei naye akaaendelea juu ya ubavu wa kile kilima, kwa kumkabili, huku akiendelea, akilaani, akimtupia mawe, na kurusha mavumbi.

Kusoma sura kamili 2 Sam. 16