Agano la Kale

Agano Jipya

Yoshua 6:16-24 Biblia Habari Njema (BHN)

16. Ilipofika mara ya saba, wakati makuhani walipokwisha piga mabaragumu, Yoshua akawaambia watu, “Pigeni kelele, kwa kuwa Mwenyezi-Mungu amekwisha wapeni huu mji!

17. Mji huo utaangamizwa na kila kitu kilichomo kwani umewekwa wakfu kwa Mwenyezi-Mungu. Rahabu, yule kahaba, ndiye atakayesalimishwa pamoja na wale ambao wamo nyumbani mwake kwa kuwa aliwaficha wapelelezi wetu.

18. Lakini msichukue chochote ambacho kimewekwa wakfu ili kiangamizwe, mkichukua kitu chochote ambacho kimewekwa wakfu ili kiangamizwe mtaifanya kambi ya Israeli kuwa kitu cha kuangamizwa, na hivyo kuiletea balaa.

19. Lakini fedha yote, dhahabu, vyombo vya shaba na chuma ni vitakatifu kwa Mwenyezi-Mungu; hivyo vitawekwa katika hazina ya Mwenyezi-Mungu.”

20. Basi, watu wakapiga kelele huku mabaragumu yanapigwa. Watu waliposikia sauti ya mabaragumu walipiga kelele kubwa, na kuta za mji zikaanguka chini kabisa. Mara watu wakauvamia mji, kila mmoja kutoka mahali aliposimama, wakauteka.

21. Kisha wakaangamiza kila kitu mjini humo na kuwaua kwa upanga: Wanaume na wanawake, vijana na wazee, ng'ombe, kondoo na punda.

22. Yoshua akawaambia wale wapelelezi wawili walioipeleleza nchi hiyo, “Nendeni katika nyumba ya yule kahaba; mkamlete yule mwanamke na wale wote ambao ni ndugu zake kama mlivyomwapia.”

23. Basi, wale vijana wapelelezi wakaenda; wakamleta Rahabu, baba yake na mama yake, ndugu zake na watu wote wa jamaa yake, wakawaweka nje ya kambi ya Israeli.

24. Kisha, wakauchoma moto mji wa Yeriko na kila kitu kilichokuwako isipokuwa fedha, dhahabu, vyombo vya shaba na vya chuma; hivyo viliwekwa katika hazina ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu.

Kusoma sura kamili Yoshua 6