Agano la Kale

Agano Jipya

Yoshua 6:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Milango ya kuingilia mjini Yeriko ilikuwa imefungwa imara kwa ndani kuwazuia Waisraeli wasiingie. Hakuna mtu aliyeweza kuingia wala kutoka katika mji huo.

2. Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, “Angalia! Mimi nitautia mikononi mwako mji wa Yeriko pamoja na mfalme wake na askari wake shujaa.

3. Wewe na wale watu wenye silaha wote mtauzunguka huo mji mara moja kila siku kwa siku sita.

4. Makuhani saba, kila mmoja akiwa amechukua baragumu yake ya pembe za kondoo dume, watatangulia mbele ya sanduku la agano. Katika siku ya saba mtauzunguka mji huo mara saba, huku makuhani wakipiga mabaragumu.

5. Watakapopiga hayo mabaragumu kwa mlio mkubwa na mara tu mtakaposikia huo mlio, watu wote watapiga kelele kubwa, nazo kuta za mji zitaanguka chini. Ndipo watu watauvamia mji kila mmoja kutoka mahali aliposimama.”

6. Basi, Yoshua, mwana wa Nuni, akawaita makuhani, akawaambia, “Libebeni sanduku la agano na makuhani saba wachukue mabaragumu saba za kondoo dume, watangulie mbele ya sanduku la Mwenyezi-Mungu.”

7. Yoshua akawaambia watu, “Nendeni mbele; uzungukeni mji, nao watu wenye silaha waende mbele ya sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu.”

8. Kulingana na amri ya Yoshua, wale makuhani saba waliokuwa na mabaragumu saba ya kondoo dume wakaenda mbele ya Mwenyezi-Mungu, wakiwa wanapiga mabaragumu, nyuma yao wakifuatwa na lile sanduku la agano.

9. Wale watu wenye silaha wakawatangulia wale makuhani ambao walikuwa wanapiga mabaragumu, na walinzi wengine wakifuata nyuma ya sanduku hilo, huku mabaragumu yakilia kwa mfululizo.

Kusoma sura kamili Yoshua 6