Agano la Kale

Agano Jipya

Yeremia 7:21-33 Biblia Habari Njema (BHN)

21. Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi: “Haya, ongezeni tambiko zenu za kuteketezwa juu ya sadaka zenu na kula nyama yake!

22. Maana, siku nilipowatoa wazee wenu nchini Misri, sikuwaambia kitu wala kuwapa amri yoyote juu ya tambiko za kuteketezwa na sadaka.

23. Lakini niliwapa amri hii: Waitii sauti yangu ili niwe Mungu wao, nao wawe watu wangu. Niliwaamuru pia waishi kama nilivyowaagiza, ili mambo yao yawaendee vema.

24. Lakini wao hawakunitii wala kunitegea sikio. Badala yake wakafuata fikira zao wenyewe na ukaidi wa mioyo yao, wakarudi nyuma badala ya kusonga mbele.

25. Tangu siku ile wazee wenu walipotoka nchini Misri hadi leo, sijakoma kuwatuma kwenu watumishi wangu, manabii.

26. Lakini hamkunisikiliza wala kunitegea sikio, ila mlizidi kuwa wakaidi, mkawa waasi kuliko hata wazee wenu.

27. “Basi, wewe Yeremia utawaambia maneno haya yote, lakini wao hawatakusikiliza. Utawaita, lakini hawatakuitikia.

28. Utawaambia; ‘Nyinyi ni taifa ambalo halikutii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, wala kukubali kuwa na nidhamu. Kwenu uaminifu umekufa; umetoweka kabisa katika maneno yenu.’

29. “Nyoeni nywele zenu enyi wakazi wa Yerusalemu, mzitupe;fanyeni maombolezo juu ya vilele vya milima,maana, mimi Mwenyezi-Mungu nimewakataa nyinyi,mlio kizazi kilichosababisha hasira yangu!

30. “Watu wa Yuda wametenda uovu mbele yangu. Wameweka vinyago vyao vya kuchukiza ndani ya nyumba hii ijulikanayo kwa jina langu, wakaitia unajisi.

31. Wamejenga madhabahu iitwayo ‘Tofethi’ huko kwenye bonde la mwana wa Hinomu, wapate kuwachoma sadaka watoto wao wa kiume na wa kike humo motoni. Mimi sikuwa nimewaamuru kamwe kufanya jambo hilo, wala halikunijia akilini mwangu.

32. Kwa sababu hiyo, siku zaja ambapo hawataliita tena ‘Tofethi,’ au ‘Bonde la Mwana wa Hinomu,’ bali wataliita ‘Bonde la Mauaji.’ Huko ndiko watakakozika watu, kwa sababu hapatakuwa na mahali pengine pa kuzikia.

33. Maiti za watu hao zitakuwa chakula cha ndege wa angani na wanyama wa porini, na hapatakuwa na mtu atakayewafukuza.

Kusoma sura kamili Yeremia 7