Agano la Kale

Agano Jipya

Yeremia 7:16-30 Biblia Habari Njema (BHN)

16. “Nawe, Yeremia, usiwaombee watu hawa, usinililie kwa ajili yao, usiwaombee dua wala usinisihi kwa ajili yao, maana sitakusikiliza.

17. Je, wewe huoni mambo wanayofanya katika miji ya Yuda na katika mitaa ya Yerusalemu?

18. Watoto huokota kuni, akina baba huwasha moto na akina mama hukanda unga ili waoke mikate kwa ajili ya mungu wa kike wanayemwita malkia wa mbinguni. Tena wanaimiminia miungu mingine tambiko ya divai ili kuniudhi.

19. Lakini je, wanamwudhi nani? Mimi? Hata kidogo! Wanajiumiza wao wenyewe na kuchanganyikiwa!

20. Kwa hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitaimwaga hasira yangu na ghadhabu yangu mahali hapa, juu ya wanadamu na wanyama, miti mashambani na mazao ya nchi. Itawaka na wala haitaweza kuzimwa.”

21. Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi: “Haya, ongezeni tambiko zenu za kuteketezwa juu ya sadaka zenu na kula nyama yake!

22. Maana, siku nilipowatoa wazee wenu nchini Misri, sikuwaambia kitu wala kuwapa amri yoyote juu ya tambiko za kuteketezwa na sadaka.

23. Lakini niliwapa amri hii: Waitii sauti yangu ili niwe Mungu wao, nao wawe watu wangu. Niliwaamuru pia waishi kama nilivyowaagiza, ili mambo yao yawaendee vema.

24. Lakini wao hawakunitii wala kunitegea sikio. Badala yake wakafuata fikira zao wenyewe na ukaidi wa mioyo yao, wakarudi nyuma badala ya kusonga mbele.

25. Tangu siku ile wazee wenu walipotoka nchini Misri hadi leo, sijakoma kuwatuma kwenu watumishi wangu, manabii.

26. Lakini hamkunisikiliza wala kunitegea sikio, ila mlizidi kuwa wakaidi, mkawa waasi kuliko hata wazee wenu.

27. “Basi, wewe Yeremia utawaambia maneno haya yote, lakini wao hawatakusikiliza. Utawaita, lakini hawatakuitikia.

28. Utawaambia; ‘Nyinyi ni taifa ambalo halikutii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, wala kukubali kuwa na nidhamu. Kwenu uaminifu umekufa; umetoweka kabisa katika maneno yenu.’

29. “Nyoeni nywele zenu enyi wakazi wa Yerusalemu, mzitupe;fanyeni maombolezo juu ya vilele vya milima,maana, mimi Mwenyezi-Mungu nimewakataa nyinyi,mlio kizazi kilichosababisha hasira yangu!

30. “Watu wa Yuda wametenda uovu mbele yangu. Wameweka vinyago vyao vya kuchukiza ndani ya nyumba hii ijulikanayo kwa jina langu, wakaitia unajisi.

Kusoma sura kamili Yeremia 7