Agano la Kale

Agano Jipya

Yeremia 44:7-18 Biblia Habari Njema (BHN)

7. “Sasa, mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, nauliza hivi: Mbona mnajiletea madhara makubwa namna hii, na kujiangamiza nyinyi wenyewe, wanaume kwa wanawake, watoto wadogo na wachanga, hata pasibaki mtu katika Yuda?

8. Kwa nini mnanichochea nikasirike kwa kuabudu sanamu mlizojitengenezea wenyewe na kuifukizia ubani miungu mingine katika nchi ya Misri ambamo mmekuja kuishi? Je, mwataka kutokomezwa na kuwa laana na dhihaka mbele ya mataifa yote duniani?

9. Je, mmesahau uovu wa wazee wenu, uovu wa wafalme wa Yuda, uovu wa wake zao na uovu wenu nyinyi wenyewe na wa wake zenu, ambao mliufanya nchini Yuda na kwenye barabara za Yerusalemu?

10. Mpaka hivi leo hamjajinyenyekesha wala kuogopa wala kuzifuata sheria zangu na kanuni zangu nilizowawekea nyinyi na wazee wenu.

11. “Kwa hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, nasema hivi: Haya! Nitawageukia niwaleteeni maafa na kuiangamiza Yuda yote.

12. Nitawaondoa watu wa Yuda waliosalia ambao wamepania kwenda kukaa Misri, na kuwaangamiza wote, wakubwa kwa wadogo; watakufa kwa upanga au kwa njaa. Watakuwa takataka, kitisho, laana na dhihaka.

13. Nitawaadhibu wale wanaokaa katika nchi ya Misri kama nilivyouadhibu mji wa Yerusalemu, kwa vita, njaa, na maradhi mabaya.

14. Kwa hiyo hapatakuwa na mtu hata mmoja kati ya watu wa Yuda waliosalia na kwenda kukaa katika nchi ya Misri ambaye atanusurika au kuishi au kurudi katika nchi ya Yuda ambayo wanatamani kurudi na kuishi humo. Hawatarudi, isipokuwa baadhi ya wakimbizi.”

15. Kisha, wanaume wote waliojua kwamba wake zao walikuwa wameifukizia ubani miungu mingine, na wanawake wote waliokuwa hapo, kusanyiko kubwa la watu, pamoja na Waisraeli waliokuwa wanakaa Pathrosi katika nchi ya Misri walimjibu Yeremia:

16. “Jambo hilo ulilotuambia kwa niaba ya Mwenyezi-Mungu hatutalitii.

17. Lakini kila kitu tulichoapa kufanya tutafanya: Tutamfukizia ubani malkia wa mbinguni na kummiminia tambiko ya kinywaji kama tulivyokuwa tunafanya sisi wenyewe na wazee wetu, wafalme wetu na viongozi wetu, katika miji ya Yuda na katika barabara za Yerusalemu. Ama wakati huo tulikuwa na chakula tele, tulistawi na hatukuona janga lolote.

18. Lakini tangu tuache kumfukizia ubani malkia wa mbinguni na kummiminia kinywaji, tumetindikiwa kila kitu, na tumeangamizwa kwa vita na njaa.”

Kusoma sura kamili Yeremia 44