Agano la Kale

Agano Jipya

Yeremia 39:4-15 Biblia Habari Njema (BHN)

4. Naye Sedekia, mfalme wa Yuda na askari wake wote walipowaona, walitoroka. Walitoka nje ya mji usiku, wakipitia katika bustani ya mfalme, kwenye lango katikati ya kuta mbili, wakaenda upande wa Araba.

5. Lakini jeshi la Wakaldayo liliwafuatia na kumteka Sedekia katika tambarare za Yeriko. Baada ya kumchukua walimfikisha kwa Nebukadneza, mfalme wa Babuloni huko Ribla, katika nchi ya Hamathi, naye akamhukumu.

6. Hukohuko Ribla, mfalme wa Babuloni aliwaua wana wa Sedekia mbele ya baba yao. Aliwaua pia maofisa wote wa Yuda.

7. Kisha alingoa macho yake Sedekia na kumfunga pingu, ili ampeleke Babuloni.

8. Wakaldayo waliichoma moto ikulu na nyumba za watu; pia walizibomoa kuta za Yerusalemu.

9. Kisha, Nebuzaradani, kapteni wa walinzi wa mfalme, aliwapeleka uhamishoni Babuloni watu waliokuwa wamebaki mjini na wale waliokuwa wamejisalimisha kwake pamoja na watu wote waliokuwa wamebaki.

10. Nebuzaradani, kapteni wa walinzi wa mfalme, aliwaacha katika nchi ya Yuda baadhi ya watu maskini ambao hawakuwa na chochote, akawagawia mashamba ya mizabibu na kuwapa maeneo ya kulima wakati huohuo.

11. Nebukadneza mfalme wa Babuloni alikuwa amempa Nebuzaradani kapteni wa walinzi, amri ifuatayo kuhusu Yeremia:

12. “Mchukue Yeremia, umtunze vema wala usimdhuru; mtendee kama anavyokuambia.”

13. Basi, Nebuzaradani kapteni wa walinzi, Nebushani, Nergal-shareza pamoja na maofisa wakuu wote wa mfalme wa Babuloni, wakatuma watu wamtoe Yeremia ukumbini mwa walinzi.

14. Wakamkabidhi Yeremia kwa Gedalia mwana wa Ahikamu, mjukuu wa Shafani, amchukue nyumbani kwake. Basi, Yeremia akaishi pamoja na wananchi wengine.

15. Neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Yeremia wakati alipokuwa amefungwa katika ukumbi wa walinzi:

Kusoma sura kamili Yeremia 39