Agano la Kale

Agano Jipya

Yeremia 33:6-18 Biblia Habari Njema (BHN)

6. “Hata hivyo, mimi nitauponya mji huu na kuwapa watu wake afya; nitawajalia ustawi mwingi na usalama.

7. Nitawastawisha tena watu wa Yuda na watu wa Israeli; nitawaimarisha kama walivyokuwa hapo awali.

8. Nitawatakasa dhambi zao zote na kuwasamehe uovu wao na uasi walionitendea.

9. Nao mji huu utakuwa sababu ya furaha kwangu, mji wa sifa na fahari mbele ya mataifa yote duniani ambayo yatasikia juu ya mema yote ninayowafanyia. Mataifa yataogopa na kutetemeka kwa sababu ya mema na fanaka nitakazouletea mji huu wa Yerusalemu.”

10. Mwenyezi-Mungu asema: “Katika mji huu ambao mnasema umekuwa ukiwa bila watu wala wanyama, naam, katika miji ya Yuda na katika barabara za Yerusalemu ambazo ni tupu, bila watu wala wanyama, humo kutasikika tena sauti za vicheko, sauti za furaha,

11. sauti za harusi na za furaha, sauti za waimbaji wakati wakileta tambiko za shukrani katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu:‘Mshukuruni Mwenyezi-Mungu wa majeshikwa kuwa Mwenyezi-Mungu ni mwema,kwa maana fadhili zake zadumu milele.’Nitairudishia nchi hii fanaka yake ya awali. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”

12. Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: “Mahali hapa ambapo ni jangwa bila watu wala wanyama, na katika miji yake yote, patakuwa na malisho ambayo wachungaji watalisha makundi yao ya kondoo.

13. Katika miji ya nchi yenye milima, katika miji ya Shefela na katika miji ya jangwa la Negebu, katika nchi ya Benyamini, kandokando ya mji wa Yerusalemu na katika miji ya Yuda, watu watahesabu tena kondoo wao. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”

14. Mwenyezi-Mungu asema: “Siku zaja ambapo nitatimiza ahadi yangu niliyofanya na watu wa Israeli na watu wa Yuda.

15. Katika siku hizo, naam, wakati huo, nitachipusha chipukizi mwadilifu wa uzao wa Daudi. Chipukizi huyo atatekeleza haki na uadilifu katika nchi.

16. Wakati huo nchi ya Yuda itaokolewa na mji wa Yerusalemu utakuwa salama. Na mji huo utaitwa ‘Mwenyezi-Mungu ni Ukombozi Wetu’.

17. Maana mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Hapatakosekana kamwe mzawa wa Daudi atakayetawala Israeli.

18. Kadhalika nao makuhani wa ukoo wa Lawi watakuwapo daima kunihudumia wakinitolea sadaka za kuteketezwa na sadaka za nafaka na kunitolea tambiko milele.”

Kusoma sura kamili Yeremia 33