Agano la Kale

Agano Jipya

Yeremia 26:13-24 Biblia Habari Njema (BHN)

13. Sasa basi, rekebisheni mienendo yenu na matendo yenu na kutii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Mkifanya hivyo, Mwenyezi-Mungu atabadili nia yake na kuacha kuwaletea maafa aliyotamka dhidi yenu.

14. Lakini mimi, tazama nimo mikononi mwenu. Nitendeeni kama mnavyoona vema na haki.

15. Ila jueni kwa hakika kwamba mkiniua, mtakuwa mmejiletea laana nyinyi wenyewe kwa kumwaga damu isiyo na hatia, na kuuletea laana mji huu na wakazi wake. Maana, ni kweli kwamba Mwenyezi-Mungu alinituma niwaambieni mambo hayo muyasikie.”

16. Hapo wakuu na watu wote wakawaambia makuhani na manabii: “Mtu huyu hastahili hukumu ya kifo, kwa kuwa amesema nasi kwa jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu.”

17. Basi, baadhi ya wazee wa nchi wakasimama na kuwaambia watu waliokuwa wamekusanyika:

18. “Wakati Hezekia alipokuwa mfalme wa Yuda, Mika wa Moreshethi, aliwatangazia watu wote kwamba Mwenyezi-Mungu wa majeshi alisema hivi:‘Mji wa Siyoni utalimwa kama shambamji wa Yerusalemu utakuwa magofu,nao mlima wa hekalu utakuwa msitu.’

19. Je, Hezekia, mfalme wa Yuda, na watu wote wa Yuda walimuua Mika? La! Badala yake Hezekia alimwogopa Mwenyezi-Mungu na kuomba fadhili zake. Naye Mwenyezi-Mungu akabadili nia yake ya kuwaletea balaa. Lakini sisi tuko mbioni kujiletea wenyewe maafa.”

20. (Kulikuwa na mtu mwingine pia aliyetabiri kwa jina la Mwenyezi-Mungu. Mtu huyo alikuwa anaitwa Uria mwana wa Shemaya, kutoka mji wa Kiriath-yearimu. Yeye alitabiri dhidi ya mji huu na dhidi ya nchi hii kama alivyofanya Yeremia.

21. Naye mfalme Yehoyakimu pamoja na mashujaa wake na wakuu wote waliposikia mambo aliyosema Uria, mfalme alitaka kumuua. Lakini Uria alipopata habari, alishikwa na hofu, akatoroka na kwenda Misri.

22. Mfalme Yehoyakimu alimpeleka Elnathani mwana wa Akbori, pamoja na watu kadhaa huko Misri.

23. Wao walimrudisha Uria kutoka Misri, wakampeleka kwa mfalme Yehoyakimu. Mfalme akamuua kwa upanga na maiti yake ikazikwa kwenye makaburi ya watu wa kawaida.)

24. Lakini Yeremia alikuwa akilindwa na Ahikamu mwana wa Shefani, ili asitiwe mikononi mwa watu na kuuawa.

Kusoma sura kamili Yeremia 26