Agano la Kale

Agano Jipya

Walawi 15:12-23 Biblia Habari Njema (BHN)

12. Chombo chochote cha udongo kilichoguswa na mtu anayetokwa na usaha ni lazima kivunjwe. Lakini chombo chochote cha mbao ni lazima kisafishwe kwa maji.

13. “Mwanamume yeyote anayetokwa na usaha akiponywa ugonjwa wake, ni lazima huyo mtu angoje siku saba kabla ya kuondolewa unajisi wake. Atayafua mavazi yake na kuoga kwa maji ya mtoni; naye atakuwa safi.

14. Siku ya nane, ni lazima alete hua wawili au makinda mawili ya njiwa mbele ya Mwenyezi-Mungu mlangoni mwa hema la mkutano na kumkabidhi kuhani.

15. Kuhani atawatoa hao, mmoja kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi na mwingine kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa; naye kuhani atamfanyia huyo mtu ibada ya upatanisho mbele ya Mwenyezi-Mungu na kumwondolea unajisi wake wa kutokwa na usaha.

16. “Kama mwanamume yeyote akitokwa na shahawa yake, ni lazima aoge mwili mzima kwa maji, naye atakuwa najisi mpaka jioni.

17. Vazi lolote lililodondokewa shahawa au ngozi yoyote iliyoguswa na shahawa hiyo ni lazima ioshwe kwa maji, na itakuwa najisi mpaka jioni.

18. Kama mwanamume akilala na mwanamke, akatokwa na shahawa, basi, ni lazima wote wawili waoge kwa maji, nao watakuwa najisi mpaka jioni.

19. “Mwanamke yeyote anapokuwa mwezini, atakuwa najisi kwa muda wa siku saba. Mtu yeyote atakayemgusa mwanamke huyo atakuwa najisi mpaka jioni.

20. Kitu chochote anacholalia au kukalia wakati yu najisi, kitakuwa najisi.

21. Mtu yeyote atakayegusa kitanda cha huyo mwanamke ni lazima ayafue mavazi yake na kuoga kwa maji; naye atakuwa najisi mpaka jioni.

22. Mtu yeyote atakayegusa kitu chochote anachokalia mwanamke huyo ni lazima ayafue mavazi yake na kuoga kwa maji, naye atakuwa najisi mpaka jioni.

23. Mwanamume yeyote atakayegusa kitu chochote alicholalia au kukalia huyo mwanamke, atakuwa najisi mpaka jioni.

Kusoma sura kamili Walawi 15